Yametimia: Patrick Aussems Atupiwa Virago, Denis Kitambi Apewa Mikoba

1st December 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania- Baada ya fununu za takribani wiki mbili hatimaye klabu ya Simba rasmi imeamua kuvunja mkataba na kocha raia wa Ubelgiji, Patrick Aussems ambaye amedumu klabuni hapo kwa msimu moja na nusu.

Patrick Aussems
Patrick Aussems
SUMMARY

Taarifa hiyo pia imegusia tukio la kocha huyo kuondoka kwenye kituo chake cha kazi bila ruhusa na hata alipoitwa kwenye kikao kwa ajili ya kujieleza alikuwa mkaidi kutoa ushirikiano uliohitajika.

Taarifa hiyo imetolewa na Aussems mwenyewe na kisha kuthibitishwa na klabu ya Simba kupitia barua iliyosambazwa kwa vyombo vya habari.

Aussems aliingia Simba mwanzo wa msimu uliopita akichukuwa nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre na kwenye kipindi chake cha kuwa kocha wa timu hiyo amefanikiwa kushinda taji la ligi kuu msimu uliopita pamoja na kuifikisha timu kwenye hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika.

Kiwango chake bora alichoonesha msimu uliopita kiliweza kuwashawishi mabosi wa Simba na waliamua kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja ambao unatarajia kuisha mwisho wa msimu huu.

Msimu huu Simba hawakuanza vizuri michuano ya ligi ya mabingwa Afrika baada ya kutolewa kwenye hatua ya mwanzo dhidi ya timu kutoka Msumbiji, UD Songo.

Hata hivyo kwenye upande wa ligi kuu bara Simba wanaongoza wakiwa na alama 25 baada ya kushuka dimbani mara 10 wakiwa wameshinda mechi 8, wamefungwa 1 na wamekwenda sare mchezo mmoja.

Mechi ya mwisho kuingoza Simba ni ile ya ligi kuu bara dhidi ya Ruvu Shooting ambapo Wekundu wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

"Bodi ya Wakurugenzi wameniambia kuwa kuwa kuanzia leo mimi siyo kocha wa Simba tena," amesema Aussems kupitia akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa Instergram.

Kumbe Tatizo Ni Nidhamu

Katika taarifa yao Simba wamesema kuwa licha ya kuwa kocha huyo kushindwa kutimiza malengo yao ya kurudi tena kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Afrika lakini waliamua kumvumilia na kuendelea kumpa ushirikiano.

Hata hivyo Simba wanasema kuwa kocha huyo alionekana kusimamia timu bila kujali malengo ya klabu yenye ari, mafanikio, nidhamu na ushindani kwenye michuano ya ndani na nje.

"Pamoja na jitihada za dhati za bodi kumpa ushirikiano kocha Aussems hata baada ya kuondoshwa kwenye michuano ya kimataifa bado kocha aliendelea kusimamia timu bila kujali malengo ya klabu yenye ari, mafanikio, nidhamu na ushindani kwenye michuano ya ndani na nje," imesomeka taarifa ya Simba.

Taarifa hiyo pia imegusia tukio la kocha huyo kuondoka kwenye kituo chake cha kazi bila ruhusa na hata alipoitwa kwenye kikao kwa ajili ya kujieleza alikuwa mkaidi kutoa ushirikiano uliohitajika.

Bodi imesema kuwa zoezi la kusaka kocha mpya atakayerithi mikoba yake limeanza mara moja lakini kwasasa Denis Kitambi aliyekuwa kocha msaidizi wa Aussems atasimamia timu kwa muda.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya