Uchambuzi: Nini Kimekwenda Tofauti Kwa Unai Emery Ndani Ya Arsenal?
30th November 2019
LONDON, Uingereza- Hayawi Hayawi, Sasa Yamekuwa! Kocha Unai Emery ameoeneshwa mlango wa kutokea ndani ya kikosi cha Arsenal baada ya kudumu kwenye kazi hiyo kwa kipindi cha miezi 18.
Mfumo huo umekuwa ukiwagharimu Arsenal na wakati mwingine kuonekana wakiruhusu mabao mepesi pindi wanapokutana na timu zenye uwezo mzuri wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza na huku zikiwa zinapress kwa nguvu.
Aliingia Arsenal kuchukuwa nafasi ya Arsene Wenger aliyedumu kwenye timu hiyo kwa miaka 22 tangu mwaka 1996.
Unai alikuja huku akiwa amebeba matumaini makubwa ya mashabiki wa Washika Bunduki wa London wakiamini pengine huenda angeweza kuwatoa kutoka sehemu moja hadi nyingine ukilinganisha na timu jinsi alivyoiacha Wenger.
Ndani ya msimu wake wa kwanza alifanikiwa kumaliza ligi akiwa kwenye nafasi ya 6 na kurudi tena kwenye michuano ya Europa kama vile alivyoachiwa na mtangulizi wake.
Kwenye kipindi chake cha miezi 18, Unai ametumia kiasi cha takribani paundi milioni 200 kwa ajili ya kuboresha kikosi kwa kusajili wachezaji mbalimbali huki Nicholas Pepe (Paund Mil 72) ukiwa ndiyo usajili wake mkubwa zaidi.
Mbali na Pepe wachezaji wengine walioingia kwa fedha nyingi ni kama vile Lucas Torreira (Paund Mil 25), William Saliba (Paundi Mil 27) ambaye atajiunga na timu msimu ujao, Bernd Leno (Paund mil 22).
SportPesa News kama kawaida tumezama na kujaribu kudadisi kuona na vitu gani hasa mbavyo vimemuangusha kocha Unai ndani ya Arsenal
Aina Ya Uchezaji
Kocha Unai alikuwa alijaribu kucheza mfumo ambao pengine ulikuwa ukiiangusha sana klabu ya Arsenal na kusababisha kukosa matokeo kwenye mechi nyingi za mashindano mbalimbali.
Tangu alipojiunga na Arsenal, Unai amekuwa akisisitiza zaidi kucheza kwa kuanzia chini wakati wakiwa wanaanzisha mashambulizi lakini kuanza kuwakabia wapinzani juu wakati wakiwa hawana umiliki wa mpira.
Mfumo huo umekuwa ukiwagharimu Arsenal na wakati mwingine kuonekana wakiruhusu mabao mepesi pindi wanapokutana na timu zenye uwezo mzuri wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza na huku zikiwa zinapress kwa nguvu.
Hata kocha alipojaribu kuimarisha ulinzi kwa kuwanunua walinzi Sokratis na David Luiz bado tatizo limeonekana kuendelea kuwepo na hivyo hiyo ilikuwa ni dalili ya kwamba mfumo huo ulikuwa hauna maana ndani ya Arsenal.
Kuamini Sana Vijana
Katika mpira wa kisasa makocha wengi wamekuwa wakiamini sana vijana lakini kwa upande wa Unai pengine vijana aliowaamini sana ilikuwa hawajafika kwenye levo kubwa ya ushindani.
Vijana 9 wamepata nafasi ya kwanza kabisa kuitumikia Arsenal chini ya Unai wakiwemo Bukayo Saka, Joe Willock, Reis Nelson na Gabriel Martinelli.
Mbali na hao waliotoka kwenye akademi ya Arsenal lakini pia mchezaji kama Matteo Guendouzi aliyesajiliwa akitoka ligi daraja la pili Ufaransa amekuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza kitu ambacho kwa namna moja ama nyingine kilikuwa kinaimaliza Arsenal taratibu.
Yuko Wapi Torreira?
Wakati anasajiliwa akitokea kwenye ligi ya Italia kunako klabu ya Sampdoria, Lucas Torreira alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuja kutuliza hali ya mambo hasa kwenye eneo la kiungo cha ulinzi cha Arsenal ambacho kilikuwa kinaonekana kuwa kina shida.
Jamaa alikuwa na takwimu bora sana kwenye ligi ya Italia na hata kwenye kombe la dunia lililofanyika Urusi mwaka jana kabla ya kujiunga na Arsenal.
Alipojiunga na Arsenal kwenye mechi za mwanzo alionekana mwiba mkali sana kwa wapinzani lakini ghafla bin vuu Torreira amepotea kwenye kikosi cha kwanza huku mimi na wewe tukiwa hatujui sababu ni nini.
Torreira amekuwa hapatikani uwanjani na hadi sasa msimu huu amecheza mechi 5 tu kati ya 13 za ligi ya Uingereza
Ishu Ya Ozil
Siyo jambo la kuficha wala kuongelea pembeni, wakati Unai anajiunga na Arsenal, mchezaji aliyekuwa na takwimu bora kabisa za kuing'arisha Arsenal alikuwa ni Mesut Ozil ama kiungo fundi kama wengi wanavyopenda kumuita.
Kiungo huyo alikuwa anarahisisha maisha ya Arsenal wakati wa kushambulia na ndiye aliyekuwa mpisha wa mabao mengi ya Arsenal kwa mujibu wa takwimu.
Kuingia kwa Unai ndiyo ilikuwa mwanzo wa kiungo huyo kuanza kukaa nje na huku sababu za msingi zikiwa hazitajwi. Sababu pekee za kiungo huyo kukaa nje alikuwa anazijua Unai.
Hali Ya Hewa Chafu
Ndani ya Arsenal inasemekana kuwa hali ya hewa ilishachafuka na ndiyo maana mabosi wa wameamua kufanya maamuzi mapema kabla ya mambo kuharibika zaidi.
Washambuliaji wao nyota kama vile Alexander Lacazette na Piere Aubameyang walikuwa washaweka wazi kwamba hawatasajili mikataba mipya kama kocha huyo ataendelea kubaki kwenye timu hiyo.
Wengi wamechoshwa na aina yake ya uongozi na hata hawakumuafiki kipindi alipomtangaza Granit Xhaka kuwa nahodha wa kikosi hicho.
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya