Riadha: Tanzania Yaambulia Patupu Kwenye Mashindano Ya Riadha Ya Dunia Qatar

7th October 2019

DOHA, Qatar- Mtanzania Alphonse Simbu ameshika nafasi ya 16 kwenye mashindano ya dunia ya riadha ambayo yamemalizika usiku wa kuamkia leo Doha nchini Qatar.

Doha, Qatar
Doha, Qatar
SUMMARY

Kushindwa kwa wanariadha hao kunaifanya Tanzania kuwa nchi pekee ya Afrika Mashariki ambayo haijapata medali hata moja kwenye mashindano hayo.

Simbu ambaye alishika nafasi ya tatu kwenye mbio hizo mwaka 2017 Jijini London, mwaka huu amemaliza katika nafasi ya hiyo ya 16 baada ya kukimbia kwa muda wa saa 2:13:57. 

Mwanariadha kutoka Ethiopia Lelisa Desisa ndiye ameibuka mshindi wa medali ya dhahabu baada ya kushika nafasi ya kwanza akitumia muda wa saa 2 dakika 10 na sekunde 40 (2:10:40) akifuatiwa na Muethiopia mwenzake Mosinet Geremew (2:10:44) huku Mkenya Amos Kipruto akikamilisha tatu bora kwa kutumia saa 2:10:51. 

Watanzania wengine ambao walishiriki kwenye mbio hizo za marathoni kwa upande wa wanaume ni Stephano Huche Gwandu na Augustine Paulo Sulle na wamekuwa ni miongoni mwa wanariadha 18 ambao hawakumaliza mbio hizo.

Kushindwa kwa wanariadha hao kunaifanya Tanzania kuwa nchi pekee ya Afrika Mashariki ambayo haijapata medali hata moja kwenye mashindano hayo.

Hapo awali, mwanadada wa Tanzania, Failuna Abdi naye alishiriki kwenye mbio ndefu lakini alijikuta akiishia njiani baada ya kuashindwa kumaliza.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya