Riadha: Caster Semenya Ahamia Kwenye Soka
6th September 2019
JOHANESBERG, Afrika Kusini -Mwanariadha bingwa mara mbili wa medali ya dhahabu kwenye michuano ya Olimpiki kwa upande wa kina dada, Caster Semenya amejiunga na timu ya mpira wa miguu ya Gauteng iliyoko Afrika Kusini.
Semenya, 28, hawezi kushindana kwenye riadha kwasasa kutokana na kubanwa na sheria ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu.
Shirikisho la Riadha Duniani, IAAF limependekeza kwamba wanariadha wenye jinsi zinazokaribiana wamekuwa na faida za ziada dhidi ya wenzao wakati wa kushindana.
Ikumbukwe kuwa jinsia ya Semenya imekuwa ni mada ambayo imezua utata huku wadau wa michezo wakihoji ni vipi mwanariadha huyo anashindana na wanawake.
Hata hivyo suala lake bado lipo mahakamani na hivyo hataweza kushiriki mashindano ya riadha ya Doha, Qatar mwezi ujao.
Mwanariadha huyo raia wa Afrika Kusini kwa sasa anafanya mazoezi kwenye timu hiyo ya Gauteng lakini hatoweza kucheza hadi mwaka 2020 kwa kutokana na kujiunga na timu hiyo ikiwa ni nje ya dirisha la usajili nchini Afrika Kusini.
"Nina furaha kuanza safari hii nyingine kwenye maisha yangu, nimepata mapokezi mazuri kwa wenzangu ndani ya timu," amesema Semenya.
Semenya si mwanariadha wa kwanza kuhamia kwenye mpira kwani bingwa wa Mita 100 wa dunia, Usain Bolt pia aligeukia kwenye soka na kujiunga na timu ya Stromsgodset ya Norway baada ya kustaafu mwaka 2017
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya