Ligi Kuu Bara: Yanga Ya Mkwasa Kuendelea Kuzoa Pointi Mbele Ya Alliance Leo?

29th November 2019

MWANZA, Tanzania- Ligi kuu soka Tanzania bara inaendelea leo kwa mchezo mmoja kupigwa ndani ya dimba la CCM Kirumba ambapo Alliance FC watakuwa wenyeji wakiwaalika Yanga ya kutoka jijini Dar es salaam.

Yanga SC
Yanga SC
SUMMARY

Kwa ujumla hadi sasa Yanga wameshinda mechi nne mfululizo za ligi kuu na ushindi kwenye mechi ya leo utakuwa ni watano wakiwa wanajaribu kujivuta kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

Alliance wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kisago cha mabao 5-0 kutoka kwa Azam kwenye mchezo wao uliopita uliofanyika siku ya Jumanne ya wiki hii.

Yanga wao wataingia wakiwa na lengo moja tu la kutaka kuendeleza wimbi lao la ushindi na kufikia mechi ya tatu mfululizo chini ya kocha wao wa muda Charles Boniface Mkwasa ambaye alichukuwa mikoba ya Mwinyi Zahera.

Kwa ujumla hadi sasa Yanga wameshinda mechi nne mfululizo za ligi kuu na ushindi kwenye mechi ya leo utakuwa ni watano wakiwa wanajaribu kujivuta kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.

Kipigo walichopata Alliance kutoka kwa Azam kilikuwa ni cha kwanza kwao msimu huu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Nyamagana lakini mechi ya leo watautumia uwanja wa CCM Kirumba kama uwanja wao.

Allience wapo nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 17 baada ya kushuka dimbani mara 12 huku Yanga wao wakiwa kwenye nafasi ya 15 wakiwa na alama 13 baada ya kushuka dimbani mara 6.

Timu hizi zinakutana uwanjani leo ikiwa ni mara ya tatu kwenye michezo ya ligi kuu bara. Kwenye michezo miwili iliyopita Yanga wameshinda mechi zote ambazo zilichezwa msimu uliopita.

Hali Ya Vikosi

Kocha wa Alliance FC, Kessy Mzirai anatarajia kuwa na kikosi chake kwa asilimia kubwa ya wachezaji kupatikana.

Hata hivyo kwa upande wa Yanga, kocha Mkwasa atalazimika kuwakosa nyota wake watano wa kikosi cha kwanza kwasababu mbalimbali.

Nyota hao ni Mohamed Issa, Feisal Salum na Abdulaziz Makame ambao wameitwa kwenye timu yao ya taifa ya Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya CECAFA mwezi ujao.

Pia mchezaji wa zamani wa Alliance aliyejiunga na Yanga mwanzo wa msimu huu, Balama Mapinduzi atakuwa nje akisumbuliwa na tatizo la nyonga huku mlinda lango Metacha Mnata akipewa mapumziko baada ya kufunga ndoa hivi karibuni.

Tumejirekebisha

Kocha Mziray wa kikosi cha Alliance amesema kuwa wamejirekebisha kutokana na makosa yaliyojitokeza kwenye mechi iliyopita dhidi ya Azam na hivyo anaamini kuwa wachezaji wake leo watacheza vizuri dhidi ya mabingwa hao wa kihistoria.

"Baada ya kufungwa mabao 5-0 na Azam tulikaa chini tukajadiliana na kuona tatizo lilikuwa wapi, nashukuru tumerekebisha kwenye mazoezi yetu ya siku mbili na leo tupo tayari kuwaonesha watu dhidi ya Yanga," amesema Mziray.

Sina Tatizo Na Molinga

Naye kocha wa Yanga, Mkwasa amesisitiza kuwa hakuna tatizo baina yake na mshambuliaji David Molinga na bado anayo nafasi ya kuendelea kumtumia kwenye mechi za ligi kuu na michuano mingine.

Mchezaji huyo alionekana kutokubaliana na maamuzi ya kocha kumfanyia sub mapema kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania siku ya Ijumaa.

Kwenye mechi hiyo Molinga alifunga bao la tatu kwa njia ya mkwaju wa adhabu kwenye kipindi cha pili na muda mfupi baada ya bao hilo alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Makame kitu ambacho alionekana kutofurahishwa nacho.

Imeandaliwa na Raheem Mohamed