Ligi Kuu Bara: Kagera Sugar Yajichimbia Kileleni, Sare Zikitawala Viwanja Vingine
22nd September 2019
MWANZA, Tanzania- Timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera imeendelea na moto waliouanza tangu mwanzo wa msimu baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 mbele ya Mbao FC ikiwa wanaendelea na rekodi yao ya ushindi asilimi 100 na kukamata usukani.
Matokeo ya sare pia yametokea kwenye michezo minne mingine ambapo Namungo ambao wamepanda daraja msimu huu na kuanza kwa kishindo wamepata sare tasa dhidi ya Mwadui FC.
Bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo uliofanyika uwanja wa Nyamagana limefungwa na Awesu Awesu kwenye dakika ya 36 kipindi cha kwanza na kuwahakikishia wakata miwa hao alama tisa wakati wakiwa wanajiandaa kuwakaribisha Simba kwenye mchezo wa ligi unaofuata.
Simba nao bado hawajadondosha alama hata moja kwenye mechi zao mbili za awali walizoshuka dimbani lakini kwa misimu mitatu iliyopita Wanamsimbazi hao wamekuwa wakilamba mchanga kila wanapokutana na vijana hao wa kocha Mecky Mexime.
Hata hivyo Simba wataingia na ahueni kidogo wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya ushindi wa 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba msimu uliopita.
Mbali na mchezo huo ambao Kagera Sugar wameibuka na ushindi, nao wakata miwa wenzao wa Morogoro, Mtibwa Sugar leo wamepata alama yao ya kwanza ya msimu baada ya kulazimisha sare ya 0-0 ugenini dhidi ya JKT Tanzania.
Hiyo inakuwa ni alama moja kwa Mtibwa msimu huu ambao wamekubali vichapo kutoka kwa Lipuli na Simba kwenye mechi zao mbili za awali.
Matokeo ya sare pia yametokea kwenye michezo minne mingine ambapo Namungo ambao wamepanda daraja msimu huu na kuanza kwa kishindo wamepata sare tasa dhidi ya Mwadui FC.
Ndanda na Singida United wametoshana nguvu ya bao 1-1 kwenye mchezo uliofanyika Nangwanda Sijaona, wageni Singida walikuwa wakwanza kufunga kupitia Frank kabla ya Ndanda kusawazisha jioni kupitia Juma Javu.
Mbeya City wameshindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani CCM Sokoine baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting.
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya