AFCON 2021: Taifa Stars Tayari Kwa Kuuzoa Alama 3 Mbele Ya Equatorial Guinea Leo

15th November 2019

DAR ES SALAAM, Tanzania - Timu ya soka ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, leo majira ya saa moja kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki Watashuka dimbani kutupa karata yao ya kwanza ya mchezo wa kundi J kuwania kufuzu Afcon

Taifa Stars
Taifa Stars
SUMMARY

Equatorial Guinea wameshinda mara moja kwenye mechi zao tano zilizopita huku wakiwa wamekwenda sara mara tatu na wamefungwa kwenye mchezo wa mwisho kushuka dimbani ambao ulikuwa ni Oktoba 20 dhidi ya Congo.


DAR ES SALAAM, Tanzania - Timu ya soka ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, leo majira ya saa moja kamili usiku kwa saa za Afrika Mashariki Watashuka dimbani kutupa karata yao ya kwanza ya mchezo wa kundi J kuwania kufuzu Afcon ya mwaka 2021 nchini Cameroon dhidi ya Equatorial Guinea.

Mpambano utapigwa uwanja wa taifa, Dar es Salaam. Huu utakuwa ni mchezo wa kwanza kwa kocha Etiene Ndayiragije tangu apewe timu kwa mkataba wa muda mrefu.

Mechi hii ni ya kwanza kwa timu hizi kukutana kwenye historia yao tangu zilipopata uwanachama wa CAF na FIFA.

Hata hivyo kuelekea mchezo huu Equatoria Guinea watakuwa wanajivunia uzoefu wao wa kushiriki michuano hii mara kwa mara ikiwemo mwaka 2015 ambapo wao walikuwa wenyeji na wakamaliza katika nafasi ya nne.

Mwaka 2012 pia timu hiyo ilifanikiwa kushiriki na kutolewa kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Ivory Coast.

Tofauti na ilivyo kwenye kikosi cha Stars ambapo tunawachezaji watatu tu ambao wanacheza nje ya bara la Afrika. Kocha wa timu hiyo Sebastien Migne ameita wachezaji 21 ambao wote wanacheza soka ulaya.

Wengi wao wanacheza kwenye nchi ya Hispania licha ya kuwa wanacheza kwenye madaraja ya chini. Federico Bikoro ni moja kati ya wachezaji hao ambaye yeye anacheza kwenye timu ya Real Zaragoza ambayo ni moja kati ya timu kongwe ndani ya La Liga ingawa kwasasa ipo daraja la kwanza.

Pedro Obiang v Mbwana Samatta

Kwenye kikosi cha Equatorial Guinea kuna kiungo anaitwa Pedro Mba Obiang ambaye kwasasa anacheza kwenye ligi ya Italia akiwa na timu ya Sassuolo inayoshika nafasi ya 13 kwenye msimamo.

Mchezaji huyo unaweza kusema ndiyo nyota zaidi wa kikosi hicho hasa ukizingatia historia yake na timu alizocheza.

Kabla ya kujiunga na Sassuolo msimu uliopita alikuwa ndani ya EPL ambapo alikuwa akikipiga ndani ya kikosi cha West Ham. 

Alizaliwa ndani ya Hispania na mpira wake wa utotoni amejivufunza kwenye akademi ya Atletico Madrid huku pia akipata nafasi ya kucheza timu ya taifa ya Hispania ya chini ya miaka 17.

Hata hivyo aliamua kuchagua kucheza timu ya wakubwa ya Equatorial Guinea ambapo leo atakwepo uwanjani dhidi ya nyota wetu Mbwana Samatta ambaye ni mshindi wa taji la ligi kuu ya Ubelgiji msimu uliopita na mshiriki wa ligi ya mabingwa msimu huu.

Fomu Ya Timu

Equatorial Guinea wameshinda mara moja kwenye mechi zao tano zilizopita huku wakiwa wamekwenda sara mara tatu na wamefungwa kwenye mchezo wa mwisho kushuka dimbani ambao ulikuwa ni Oktoba 20 dhidi ya Congo.

Stars nao kwenye michezo mitano iliyopita, wamesinda mara moja, sare tatu na wamefungwa mara moja.

Rekodi Mbovu Ugenini

Equatorial Guinea wanarekodi ya kucheza mechi 48 ugenini bila kushinda mchezo hata mmoja. Kama Stars watatumia mwanya huo wanaweza kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo.

Ndayiragije Atoa Neno

Nimeteua kikosi bora ambacho naamini kitawapa furaha mashabiki wetu ni mchezo mgumu lakini nimewasoma vizuri wapinzani sidhani kama watatusumbua sana licha ya kikosi chao kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka Ulaya hasa Hispania, amesema Ndayiragije.

Migne Atamba Kuijua Stars

Nawajua vizuri Tanzania nimecheza nao mara mbili nikiwa kocha wa Kenya mara ya kwanza niliwafunga 3-2 kule Misri kwenye Afcon na wao walinitoa kwa penati kwenye kufuzu fainali za CHAN kwahiyo siyo timu ngeni nawajua na tegemezi wao ni Samatta, amesema Migne.

Mechi Nyingine:

Tunisia v Libya

Zimbabwe v Botswana

Morocco v Mauritania

Imeandaliwa na Raheem Mohamed