Uchambuzi: Vitu Vitano Alivyosema Mwakinyo Baada Ya Kumpiga Mfilipino

30th November 2019 - by Adam Mbwana

DAR ES SALAAM, Tanzania- Bondia Hassan Mwakinyo amefanikiwa kushinda kwa pointi kwenye pambano lake la kimataifa alilipigana dhidi ya mkali kutoka nchini Uphilipino, Arnel Tinampay.

Hassan Mwakinyo
SUMMARY

"Nilikuwa nakaa kwenye kamba kwasababu nilikuwa nataka kupima punch za mpinzani wangu lakini pia kutumia kamba zile na mimi nilikuwa napata nafasi ya kuingiza makombora yangu kwenye uso wa jamaa," amesema Mwakinyo.

Mara baada ya pambano hilo Mwakinyo ameongea na waandishi wa habari na hizi hapa kauli tano alizosema

Sijaridhika Na Ushindi

Katika mahojiano hayo Mwakinyo amesema kuwa kama ilivyo kwa watanzania wengi ambao hawajiridhika na ushindi huo hata yeye pia hajaridhika kwani alipanga kufanya kitu kikubwa zaidi ya pale.

"Nilipanga kufanya kitu kikubwa ikiwezekana kushinda kwa KO lakini nimekutana na mpinzani ambaye ni mzuri na mvumilivu sana kitu ambacho kimefanya pambano kuwa gumu kuliko nilivyotegemea,"

Amsifu Tinampay

Mwakinyo amesema kuwa Tinampay ni bondia mzuri sana hasa ukizingatia anatoka kwenye kambi ya Manny Pacquiao. Amesema kuwa mpinzani wake huyo alikuwa anacheza kwa kasi sana na ni mwepesi wa kuona mapungufu ya adui yake.

Alia Kuvuliwa Gloves

Mwakinyo amelalamikia kitendo cha kulazimishwa kuvuliwa gloves zake alizozizoea na badala yake kuvalishwa nyingine ambazo hajawahi kuzitumia kwenye mapambano yake mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

"Kama uliona pambano lilichelewa kuanza ni kwasababu jamaa walinitaka kuvua gloves zangu zenye nembo ya SportPesa ambazo mimi ndiyo nimezoea kuzivaa kwenye mapambano yangu mbalimbali"

"Kitendo cha leo kuvalishwa gloves nyingine kwa namna moja ama nyingine kilinirudisha nyuma kimbinu na ndiyo maana sikuchangamka kwenye mechi," amesema Mwakinyo.

Kukaa Kwenye Kamba Ni Mbinu

Mwakinyo amesema mchezo wa ngumi na kama michezo mingine ambapo wachezaji huwa wanambinu zao mbalimbali za kutafuta matokeo.

Amesema hivyo akiwa anaitetea staili yake ambayo ameitumia muda mrefu ya kuegemea kamba kitendo ambacho kilikuwa kinampa nafasi Tinampay kushambulia mfululizo.

"Nilikuwa nakaa kwenye kamba kwasababu nilikuwa nataka kupima punch za mpinzani wangu lakini pia kutumia kamba zile na mimi nilikuwa napata nafasi ya kuingiza makombora yangu kwenye uso wa jamaa," amesema Mwakinyo.

Ataka Mabondia Wakubwa Zaidi

Mwakinyo ametoa mwito kwa makampuni makubwa kama ilivyo SportPesa kudhamini michezo ya ngumi nchini ili kuweza kuikuza na siku za baadaye mabondia wakubwa kama vile Amir Khan na Manny Pacquiao waweze kuja nchini.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya