Uchambuzi Ligi Kuu Bara: Nani Waliopatia Kutimua Kocha, Nani Waliobugi?

11th November 2019 - by africanus panga

Ligi kuu Tanzania Bara ipo kwenye mzunguko wa 10 kwa baadhi ya timu ingawa kuna timu zimecheza mechi chache na hazijafika idadi hiyo.

Mwinyi Zahera
SUMMARY

Yanga nao hivi karibuni wametimua kocha, wamemfukuza Mwinyi Zahera akiwa ameisimamia timu kwenye mechi nne tu akishinda mbili, akifungwa moja na kwenda sare mchezo mmoja.

DAR ES SALAAM,Tanzania -Ligi kuu Tanzania Bara ipo kwenye mzunguko wa 10 kwa baadhi ya timu ingawa kuna timu zimecheza mechi chache na hazijafika idadi hiyo.

Hata hivyo licha ya kuwa kwenye hatua za mwanzoni tu naweza kusema lakini tayari kuna baadhi ya timu ambazo zimeshaamua kubadili makocha kwasababu mbalimbali lakini kubwa ikiwa ni matokeo.

Kwenye kapu hili siwezi kumuingiza aliyekuwa kocha wa Azam, Ettiene Ndayiragije ambaye yeye baada ya kuanza msimu akiwa na Wana Lambalamba lakini alikuja akajiondoa hapo kwa makubaliano maalumu na sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Tanzania.

Ukiachana na yeye, zipo timu sita nyingine ambazo zimefanya mabadiliko hayo ya benchi la ufundi. Swali linabaki ni je timu ipi imefanya maamuzi sahihi na timu ipi ilikosea kutimua kocha.

Kikawaida timu inapofanya vibaya lawama zote huwa ni kwa kocha lakini kuna wakati kufanya vibaya kwa timu chimbuko lake linaanzia mbali si tu kwenye benchi la ufundi na wachezaji.

Na kwasababu hiyo ndiyo maana kuna timu zikibadili kocha na matokeo yanakuwa mazuri na nyingine hata zikibadili kocha matokeo yanaendelea kuwa mabaya tena pengine kushinda hata yale ya awali.

Felix Minziro (Singida United)

Singida United ni miongoni mwa timu za mwanzo kutimua kocha, walifanya hivyo tangu kwenye mechi ya nne tu ya msimu ambapo walimtimua Felix Minziro na nafasi yake kuchukuliwa na Mrundi, Ramadhan Nswanzerimo.

Wakati Minziro anaondoka timu ilikuwa haiwajawahi kupata ushindi kwenye mechi zake nne za awali na hadi kufikia sasa timu inaburuza mkia ikiwa imecheza mechi 11 na haijawahi kupata ushindi chini ya kocha wao mpya. (Maamuzi siyo sahihi)

Malale Hamsini (Ndanda FC)

Malale Hamsini alifukuzwa Ndanda baada ya kuisimamia timu kwenye mechi sita huku ikiwa haijashinda mchezo hata mmoja na ikiwa kwenye nafasi ya 19.

Aliyekuja kuchukuwa mikoba yake ni Shaweji Nawanda ambaye naye licha ya kuiwezesha timu kushinda kwenye mechi moja lakini bado wapo nafasi ya 19 wakiwa na alama 7 ndani ya mechi 9. (Maamuzi Siyo Sahihi)

Athuman Bilal (Allience)

Huyu ndiye alikuwa muhanga wa kwanza kukutana na rungu la kufukuzwa. Alifukuzwa baada ya kumalizika mchezo wa kwanza tu wa ligi baada ya kupokea kichapo kutoka kwa Mbao

Aliyechukuwa nafasi yake ameingoza timu kwenye mechi michezo tisa wakishinda mara tatu, wakienda sare mara mbili na wamefungwa mara moja tu chini ya kocha mpya. wana alama 14. (Maamuzi sahihi)

Mwinyi Zahera (Yanga)

Yanga nao hivi karibuni wametimua kocha, wamemfukuza Mwinyi Zahera akiwa ameisimamia timu kwenye mechi nne tu akishinda mbili, akifungwa moja na kwenda sare mchezo mmoja.

Mtu aliyechukuwa nafasi yake amekaimu kwa muda na ameongoza timu kwenye mchezo mmoja wa ugenini dhidi ya Ndanda ambapo Yanga walishinda 1-0. (Muda Bado)

Jackson Mayanja (KMC)

Baada ya kuondoka kwa Etiene Ndayiragije, KMC walitafuta tena kocha wa nje ya nchi na safari hii walifika Uganda ambapo walimkuta Jackson Mayanya ambaye wakati fulani aliwahi kufanya kazi Simba.

Mayanja ameisimamia timu tangu mwanzo wa ligi akiwa kama kocha ndani ya mechi 8. Lakini tofauti na matarajio ya wengi, matokeo yalikuwa si kama wengi walivyodhania hasa ukiangalia uwekezaji uliofanyika kwenye kikosi.

KMC ina alama 8 ndani ya mechi na mechezo wa mwisho kwa Mayanja ulkuwa ni ule wa Alhamis ambapo walifungwa 2-1 na Kagera Sugar wakiwa uwanja wao wa nyumbani. Bado mrithi hajatajwa. (Muda Bado)

Amri Said (Biashara United)

Kocha Amri Said alianza msimu wa ligi akiwa kama kocha wa Biashara United lakini baada ya mechi 4 tu alitimuliwa baada ya timu kufungwa michezo yote chini yake.

Aliyemfuatia ameongoza timu kweye mechi 6 akishinda mara mbili sare mbili na kufungwa mara mbili, wamecheza jumla mechi 10 na wapo nafasi ya 17 kwenye msimamo wakiwa na alama 8. (Maamuzi Sahihi)

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya