Riadha: Mkenya Mwingine Aweka Rekodi Ya Dunia Kwenye Marathoni Nchini Marekani
14th October 2019
CHICAGO, Marekani- Siku mbili baada ya Mkenya, Eliud Kipchoge kuweka rekodi ya dunia kwenye mbio za marathon akitumia chini ya saa mbili kukimbia umbali wa kilometa 42, Mkenya mwingine ameweka rekodi ya dunia kwa upande wa wanawake.
Kwenye mashindano hayo ya Chicago ambapo Kosgei ameweka rekodi, Ababel Yeshaneh raia wa Ethiopia aliibuka kwenye nafasi ya pili akizidiwa dakika 6 na sekunde 47.
Brigid Kosgei, 25, ameweka rekodi yake ya dunia kwenye mbio za marathoni baada ya kutumia muda wa saa 2:14:04 akiivuka rekodi ya saa 2:15:25 iliyowekwa na Muingereza, Paula Radcliffe aliyoweka wakati wa mashindano ya marathoni yaliyofanyika London, Uingereza, 2003.
Kosgei ameweka rekodi hiyo wakati wa mashindano ya marathon yaliyofanyika Chicago, Marekani ambapo pia yeye alikuwa anashikilia ubingwa wa michuano hiyo na hivyo jana amefanikiwa kutetea taji lake.
Mapema mwaka huu pia kwenye mashindano ya London, Kosgei alishinda taji akimaliza kwa muda wa saa 2:18:20 na kuwa bingwa mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutokea kwenye michuano hiyo.
Kwenye mashindano hayo ya Chicago ambapo Kosgei ameweka rekodi, Ababel Yeshaneh raia wa Ethiopia aliibuka kwenye nafasi ya pili akizidiwa dakika 6 na sekunde 47.
"Ninajisikia vizuri sana kwasababu sikutegemea kama nitakimbia kwa kiwango hiki cha kusisimua," amesema Kosgei.
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya