Rasmi: Adam Salamba Atimkia Kuweit

8th September 2019 - by Adam Mbwana

INSTANBUL, Uturuki -Aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Adam Salamba amekamilisha dili lake la kujiunga na klabu ya Al-Jahra ya nchini Kuweit kwa mkataba wa miaka mitano. Mkataba huo amesaini nchini Uturuki ambako timu hiyo imeweka kambi kujiandaa na msimu mpya unaotarajia kuanza hivi karibuni. Akizungumza na SportPesa News, Salamba amesema amekubali kusaini mkataba huo baada ya kuvutiwa na ofa aliyoahidiwa ambayo pia imeinufaisha na klabu yake ya Simba. Salamba ameondolewa kwenye kikosi cha Simba, kutokana na kukosa namba ya kudumu kwenye kikosi hicho msimu uliopita chini ya kocha Patrick Aussems na kulazimika kuondolewa ili kutafuta sehemu ambayo atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Salamba anaongeza idadi ya wachezaji wakulipwa wanaocheza soka nje ya Tanzania ambao wanaongozwa na nahodha Mbwana Samatta, Farid Mussa, Simon Msuva, Ally Ng’azi na wengineo. Imeandaliwa na Rahim Mohamed.