Ligi Kuu Bara: Haya Ndio Mambo Makubwa Matano Yaliyojiri Mechi Ya Simba v Azam Jana
24th October 2019
DAR ES SALAAM, Tanzania -Mechi ya iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini ikiwakutanisha Simba na Azam imefanyika ambapo kama kawaida wekundu wa msimbazi wamejimwambafay kwa kuibuka na ushindi wa 1-0.
Mara baada ya mchezo huo Cheche alisema kuwa licha ya kujipanga vilivyo na wachezaji wake kujituma sana uwanjani lakini bado wamefungwa na Simba na hicho ndo kilimfanya akubali kuwa timu hiyo ni kiboko kwasasa hapa nchini.
Shujaa wa mchezo huo alikuwa ni mshambuliaji Meddie Kagere ambaye alifunga bao la ushindi kunako kipindi cha pili na kumfanya azidi kujikita kileleni kwenye orodha ya wafungaji bora akiwa na mabao 7.
Mambo kadhaa kuhusu mchezo huo yameshazungumzwa sana lakini kwa kifupi SportPesa News inakukusanyia makubwa matano yaliyojiri ndani na nje ya uwanja.
Simba Yajimwambafay Mbele Ya Azam
Kama unakumbuka mchezo wa kukata utepe wa ligi msimu huu ulikuwa ni kati ya Simba na Azam na wekundu wa msimbazi walishinda 4-2.
Ushindi wa jana kwa Simba umekuwa ni kama muendelezo wa ubabe wao dhidi ya Azam ambao kwa miaka ya karibuni wamekuwa adimu kupata matokeo ya ushindi mbele ya wekundu wa msimbazi.
Ufundi Watawala
Licha ya Simba kuibuka na ushindi lakini mchezo wa jana ulitawaliwa na ufundi mwingi kiasi chake.
Wachezaji wa pande zote mbili walikuwa wakijaribu kuoneshana uhodari wao wa kusakata gozi la ng'ombe kitu ambacho kiliamsha shangwe nyingi kwa mashabiki kiduchu waliojitokeza uwanjani.
Kwa upande wa Azam, Abuubakar Salum na Mudathir Yahaya walikuwa moto balaa huku Francis Kahata na Muzamiru Yassin wakionesha uhodari wao kwa upande wa Simba.
Undava Wachukuwa Nafasi
Licha ya mchezo huo kujawa na ufundi lakini pia kulikuwa na vita kubwa ya kutunishiana misuli baina ya timu zote mbili.
Wachezaji wa pande zote walionesha hali ya kupaniana na kuchezeana rafu nyingi zisizo za kiungwana kitu kilichomfanya mwamuzi wa mchezo huo kutembeza kadi za njano kama njugu.
Cheche Ainua Mikono
Kocha msaidizi wa Azam, Idd Cheche alikuwa kwenye bechi la ufundi jana akiwaongoza Azam kufuatia kuondokewa na kocha wao Etiene Ndayiragije.
Azam wameshamsajili kocha mpya Aristica Cioaba lakini hakuanza kazi jana kwakuwa bado hana vibali vya kufanyia kazi.
Mara baada ya mchezo huo Cheche alisema kuwa licha ya kujipanga vilivyo na wachezaji wake kujituma sana uwanjani lakini bado wamefungwa na Simba na hicho ndo kilimfanya akubali kuwa timu hiyo ni kiboko kwasasa hapa nchini.
Meddie Kegere v Obrey Chirwa
Kwenye mchezo wa jana kila timu ilikuwa na matumaini kwa wachezaji wao nyota wanaocheza kwenye nafasi ya ushambuliaji.
Azam waliweka matumaini yote kwa Chirwa na almanusura afunge bao kipindi cha kwanza baada ya kugongesha mwamba.
Hata hivyo Simba walikuwa sahihi kuweka matumaini yao kwa Kagere ambaye ndiye aliyewasaidia kuzoa alama zote tatu baada ya kukwamisha mpira wavuni kwa kutumia kichwa kunako dakika 49 ya mchezo akiunganisha pasi ya Francis Kahata.
Imeandaliwa na Rahim Mohamed