Kombe La Shirikisho: Za Moto Moto Tano Zilizojiri Kirumba Yanga v Pyramids
28th October 2019
MWANZA, Tanzania- Yanga jana wamefungwa nyumbani na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonge mbele hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga jana walianza na mfumo ambao ulikuwa unajumuisha viungo wa kati takribani wanne na mshambuliaji wa kati mmoja tu Sadney Urikhob huku winga pekee akiwa ni Mrisho Ngasaa.
Kutokana na mfumo huo Yanga hawakuweza kuwabugudhi wageni hata kidogo huku kikiwa ndio chanzo hata cha kufungwa.
Kwenye mchezo huo kulikuwa na mengi yaliyojiri lakini makubwa ni haya yafuatayo kama yanavyoletwa kwenu na SportPesa News.
Zomea Zomea
Hili ni moja kati ya matukio yaliyogubika uwanja wa CCM Kirumba jana ambapo mashabiki ambao walikuwa hawajaridhishwa na timu yao walianza kuzomea baadhi ya wachezaji pamoja na zomea nyingine zikielekezwa kwa kocha Mwinyi Zahera.
Wengine walifika mbali zaidi na kuanza kumrushia chupa za maji kocha huyo mara baada ya kipyenga cha mwisho na wengi wakishinikiza uongozi kwamba kocha huyo atimuliwe.
Mfumo Waigharimu Yanga
Licha ya kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila kutetea mfumo walioutumia jana lakini ni wazi kabisa uliwagharimu.
Yanga jana walianza na mfumo ambao ulikuwa unajumuisha viungo wa kati takribani wanne na mshambuliaji wa kati mmoja tu Sadney Urikhob huku winga pekee akiwa ni Mrisho Ngasaa.
Kutokana na mfumo huo Yanga hawakuweza kuwabugudhi wageni hata kidogo huku kikiwa ndio chanzo hata cha kufungwa.
Makame ni bonge la mido
Tangu alipojifunga bao pale Ndola, Zambia dhidi ya Zesco nimekuwa nikimfuatilia kiungo Abdulaziz Makame kuona kama tukio lile linaweza kuathiri kiwango chake kwa kiasi gani.
Hata hivyo inaonesha kijana huyo alishayaacha yale yapite na amekuwa akicheza kwa kiwango kikubwa karibia kila mechi ikiwepo ile ya jana.
Kwa mchezo dhidi ya Pyramids naweza kusema kuwa jambo zuri pekee analoweza kulichukuwa kocha ni kiwango cha Makame kwenye mchezo huo.
Mlima Wa Majeruhi
Yanga wanamlima wa wachezaji majeruhi na wengine waliokosa leseni. Kutokana na hivyo kocha Zahera jana alitaja walinda mlango wawili kwenye benchi lake kitu ambacho si cha kawaida.
Mchezo wa marudiano utakuwa mgumu zaidi kwao kama baadhi ya wachezaji hawatarudi kwani tayari hadi sasa wana uhakika wa kuwakosa walinzi wao tegemeo Kelvin Yondani na Lamine Moro ambao wote wana kadi nyekundu.
Mil 30 Za GSM Zayeyuka
Kama ilivyo kwenye mechi za ligi kuu ambapo kampuni ya GSM ambayo ndiyo wasambazaji wa jezi za Yanga huwa wananunua pointi 3 kwa shilingi milioni 10.
Tangu utaratibu huo ulipoanza Yanga walishinda mechi zao mbili dhidi ya Coastal Union na Mbao na walifanikiwa kubeba kitita hicho.
Hata hivyo kwenye mchezo wa jana licha ya kuwa wamezidishiwa dau na kufika milioni 30 lakini bado Yanga hawakuweza kuupanda mlima mrefu dhidi ya waarabu na sasa hela hizo zimerudi kwa wenyewe.
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya