Kelvin John Atimkia Genk Kuungana Na Samatta
13th September 2019
DAR ES SALAAM, Tanzania- Kinda wa timu ya Taifa ya Tanzania Taifa stars Kelvin John, usiku wa jana amesafiri kuelekea nchini Ubelgiji, kuitika mualiko wa klabu ya KRC Genk anayochezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta
Kelvin John ameng'aa akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 ambacho kilikuwa mwenyeji kwenye fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo zilizofanyika jijini Dar es Salaam
Kelvin (16) alitumiwa mualiko na klabu hiyo yenye timu yake inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza nchini humo Julai 25 mwaka huu.
Kwa mujibu wa mualiko huo, inaelezwa kuwa kinda huyo wa Taifa stars atasaini mkataba na makubaliano mwezi huu wa Septemba ingawa ataanza kazi rasmi uwanjani Januari mwakani.
Mualiko huo ulieleza kuwa gharama za safari ikiwemo malazi, chakula na bima vitagharamiwa na klabu ya Genk.
Kelvin ni miongoni mwa wachezaji vijana wenye ushawishi wa soka kwa sasa nchini na amaekuwa akifananishwa na mshambuliaji kinda wa Ufaransa na PSG, Kylan Mbappe.
Mweji Juni, alijumuishwa kwenye kikosi cha awali kikichotarajiwa kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon) lakini baadaye alianguliwa baada ya aliyekuwa kocha mkuu Emmanuel Amunike kutangaza kikosi cha mwisho chenye wachezaji 23.
Imeandaliwa na Badrudin Yahaya