ATP: Novak Djokovic Na Rodger Federer Watupwa Kwenye Kundi Moja Huko London

6th November 2019 - by Adam Mbwana

LONDON, Uingereza- Wachezaji tenesi nyota kwa upande wa wanaume, Rodger Federer na Novak Djokovic wamepangwa kundi moja la michuano ya dunia ya mchezo huo ambayo imepangwa kuanza kutimua vumbi Jumapili ijayo nchini Uingereza.

Novak Djokovic
SUMMARY

Hata hivyo Djokovic anayo nafasi ya kurudi tena kileleni endapo atafanikiwa kumaliza akiwa bingwa wa michuano hii ya London huku akimuombea Nadal asifike hatua ya nusu fainali.

Nguli hao wa mchezo huo wamepangwa sambamba na Dominic Thiem pamoja na matteo Berrettin.

Naye mchezaji namba moja kwa ubora duniani, Rafael Nadal amepangwa kwenye kundi ambalo ndani yake wapo Daniil Medvedev, Stafanos Tsitsipas na Alexander Zverev.

Mapema wiki hii Nadal alisema kuwa amelenga kushiriki michuano hiyo ya London japokuwa alijiengua kwenye michuano ya Paris Masters kwa madai ya kuwa majeruhi.

Mhispania huyo amesema kuwa vipimo vya MRI vimeonesha kuwa alikuwa na tatizo dogo tu kwenye mishipa yake.

Ingawa hakushiriki michuano hiyo ya Paris, lakini Nadal alifanikiwa kumpiku Djokovic kileleni kwenye viwango vya ubora kwa upande wa wanaume.

Hata hivyo Djokovic anayo nafasi ya kurudi tena kileleni endapo atafanikiwa kumaliza akiwa bingwa wa michuano hii ya London huku akimuombea Nadal asifike hatua ya nusu fainali.

ATP ni mashindano ya mwisho ya msimu wa tenesi ambayo yanajumuisha wachezaji nane kwa ubora duniani ambao wanagawanywa kwenye makundi mawili.

Wachezaji watakaomaliza nafasi mbili za juu kutoka kwenye makundi hayo mawili wanaingia nusu fainali.

Imeandaliwa na Badrudin Yahaya