SportPesa XI: Nyota Ligi Ya Uingereza Wagombea Nafasi Kwenye Timu Ya Wiki

11th November 2019

LIVERPOOL, Uingereza- Ligi Kuu ya Uingereza imefikia mzunguko wa 12 wikendi iliyoisha baada ya timu zote kushuka dimbani katika viwanja tofauti.

Ben Foster
Ben Foster
SUMMARY

Manchester United, Chelsea, Leicester City mambo yalikuwa mazuri kwa upande wao ila hofu inazidi kuwa juu kwa makocha Unai Emery na Mauricio Pochettino ambapo timu zao bado zimeendelea kuambulia patupu kwenye michezo ya ligi.

LIVERPOOL, Uingereza -Ligi Kuu ya Uingereza imefikia mzunguko wa 12 wikendi iliyoisha baada ya timu zote kushuka dimbani katika viwanja tofauti.

Tukiwa tunaingia kwenye mapumziko mengine ya timu za taifa, Liverpool ndiyo timu pekee imebaki ikiwa bado haijapoteza mchezo, hiyo ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao wakubwa kwenye michuano hiyo Manchester City.

Manchester United, Chelsea, Leicester City mambo yalikuwa mazuri kwa upande wao ila hofu inazidi kuwa juu kwa makocha Unai Emery na Mauricio Pochettino ambapo timu zao bado zimeendelea kuambulia patupu kwenye michezo ya ligi.

SportPesa News tunakuletea kikosi bora cha wiki cha Ligi Kuu ya Uingereza ambapo kwa mujibu wa upangaje wake mfumo utakuwa ni 3-4-3.

Kipa: Ben Foster (Watford)

Kiwango cha Ben Foster kwa wiki hizi mbili kimekuwa kikubwa sana pengine huwezi kumlinganisha na kipa mwingine yeyote ndani ya EPL kwasasa.

Hiyo ndiyo imetufanya na sisi kumuweka ndani ya kikosi hiki kwa wiki ya pili mfululizo.

Kama alivyokuwa muhimili kwenye mechi iliyopita dhidi ya Chelsea, Foster alikuwa bora tena dhidi ya Norwich ugenini ambapo aliiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa 2-0 na ni ushindi wao wa kwanza kabisa msimu huu.

Mabeki: Ricardo Pereira (Leicester)

Mafanikio ya Leicester City msimu huu unaweza kusema kuwa yanachangiwa sana na walinzi wake wapembeni, Ricardo Perreira na Bem Chilwell.

Kwenye mechi dhidi ya Arsenal ambapo Foxes walishinda 2-0, Perreira alikuwa bora sana kila alipokwenda mbele na alipiga pasi 21 ndani ya eneo la hatari kitu ambacho hakuna mwingine aliyeweza kufanya.

Federico Fernandez (Newcastle)

Ni mmoja kati ya walinzi hodari ndani ya kikosi cha Newcastle United. Alikuwa kwenye wakati mzuri akiwadhibiti washambuliaji wa Bournemouth wakiongozwa na Joshua King na hadi kuiwezesha timu yake kushinda kwa mabao 2-1.

Chris Basham (Shefield United)

Sheffield United ni moja kati ya timu ngumu sana kupitika kwenye safu yake ya ulinzi lakini isingekuwa rahisi bila ya uwezo wa Chris Basham.

Basham aliweza kuwakabili washambuliaji wa Spurs wikiendi hii na kuwafanya waonekana si lolote na hadi timu hiyo kupata sare ya 1-1 ndani ya White Hart Lane.

Viungo: Ruben Neves (Wolves)

Kwenye mechi dhidi ya Aston Villa Reuben Neves alikuwa muhimili mkubwa katika eneo la kiungo cha kujilinda na kuifanya safu ya ulinzi ya Wolves kuwa na wakati mzuri sana sababu mipira mingi Neves aliiokoa kabla ya kumfikia mlinda mlango.

Mchango wake huo uliisaidia timu kupata ushindi wa 2-1.

Fabinho (Liverpool)

Kiwango bora cha Fabinho ndiyo kikwazo kwa vijana wa Man City kushindwa kuibuka na ushindi kwenye mechi ya jana.

Kuna muda aliwapoteza kabisa viungo wa Man City ambao waliianza mechi vibaya. Bao alilofunga ni zuri na ukizingatia yeye si mfungaji wa mara kwa mara.

Tom Davies (Everton)

Kukosekana kwa Andrew Gomes aliyeumia vibaya wiki iliyopita, kumemfanya Tom Davies kupata nafasi kwenye kikosi cha Everton dhidhi ya Southampton.

Mechi hiyo ilishiisha kwa Everton kushinda 2-1 lakini chaguo la Davis kikosini halikumuangusha kocha Marco Silva hata kidogo.

Willian (Chelsea)

Willian kwa sasa ndiye kama kiongozi katika kikosi cha Chelsea chenye vijana wengi.

Mbrazil huyo dhidi ya Crystal Palace alipewa kitamba cha unahodha na alikitendea haki kwa kuonesha ubora mkubwa alitengeneza uelewano mzuri mbele pamoja na Abraham na Pulisic na kuiwezesha timu kushinda 2-0 huku akitengeneza bao moja

Washambuliaji: Jamie Vardy (Leicester)

Jamie Vardy ndiye kinara wa mabao kwa sasa akiwa na mabao yake 11 katika michezo 12.

Kwenye mchezo dhidi ya Arsenal licha ya kuwa chini ya ulinzi mkali wa David Luiz aliweza kufunga bao safi na kama angekuwa makini angefunga na mengine ya ziada.

Christian Pulisic (Chelsea)

Tangu alipofunga hat trick kwenye mechi dhidi ya Burnley, ni wazi kabisa Mmarekani huyo ameanz kufurahia wakati wake mzuri ndani ya Stamford Bridge.

Bao alilofunga dhidi ya  Palace juzi ni la tano kwenye michezo mitatu iliyopita ya ligi.

Gerard Deulofeu (Watford)

Huyu ndiye unaweza kusema kuwa ni nyota wa Watford kwasasa. Anafunga na kutengeneza nafasi kwa wenzake.

Kwenye ushindi waliopata dhidi ya Norwich siku ya Ijumaa isingewezekana kama siyo mchango wa Deulofeu ambaye alifunga bao moja kama kawaida yake.

Kocha: Jurgen Klopp (Liverpool)

Ni wazi kabisa kazi ya kocha Jurgen Klopp ni nzuri sana na timu yake imekuwa ikicheza kwa nidhamu kubwa.

Sijajua mbele kitatokea nini lakini ni jambo ambalo si la kupinga kwamba Klopp ametengeneza timu ya ubingwa msimu huu.

Imeandaliwa na Jery Mlosa