Connect with us

Habari

“Tunaiheshimu Yanga Ingawa Dakika 90 Zitazungumza”, Kocha Kakamega Atamba.

Spread the love

NAKURU, Kenya -Kocha Mkuu wa Kakamega Homeboyz, Paul Nkata amesema wanawafahamu vyema wapinzani wao, Yanga na wanaheshimu kwa kiasi kikubwa.

Yanga ambao ni mabingwa mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara watakata utepe wa michuano ya SportPesa Super Cup kwa kuwavaa Kakamega Homeboyz kwenye dimba la Afraha majira ya saa 7 kamili mchana wa leo.

Akizungumza na wana habari kwenye hoteli ya Ole Ken hapo jana Juni 2, Nkata ambaye amewahi kuifundisha Tusker FC ya nchini hapa amekiri kuwa Yanga ni timu kubwa ukilinganisha na timu yao lakini hilo haliwazuii kucheza mpira wao wa kawaida.

“Tunajua Yanga ni timu kubwa kwenye ukanda huu wa Afrika mashariki tofauti na sisi (Kakamega) na tunaliheshimu hilo ingawa siku zote mpira ni dakika 90 na baada ya mechi tutajua nani ni mbabe wa mwenzake uwanjani”, alisisitiza.

Kikosi cha Kakamega kikifanya mazoezi Juni Mosi kuelekea kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga (Picha-SPN)

Tutashambulia tu

Aidha kocha huyo raia wa Uganda ambaye ameipa Tusker ubingwa wa Kenya mwaka 2016 amesema ataingia kwenye mchezo wa Yanga akiwa na lengo la kushambulia tu huku akijivunia uwepo wa mshambuliaji Alan Wanga ambaye amewahi kuchezea Azam FC.

“Tunataka kuhakikisha tunacheza mfumo wa kushambulia dakika zote 90 kwasababu kwenye mchezo wa soka ili uweze kushinda ni lazima ufunge magoli na ili uweze kufunga ni lazima ushambulie hivyo nataka kuona ni jinsi gani kikosi changu kitaweza kulifanikisha hilo”, alisema.

Hata hivyo kocha huyo ambaye pia amewahi kuvifundisha vilabu vya Muhoroni Youth na Bandari vya nchini hapa amekiri kuwa kucheza dhidi ya timu za Tanzania kutaipa uzoefu mkubwa timu yake.

“Kucheza na timu za Yanga na Simba zitatupa changamoto kubwa na pia tutaweza kujua jinsi wanavyocheza kwasababu kama unavyojua soka la Tanzania ni tofauti kabisa na soka la Kenya”, alihitimisha Nkata.

Siahidi chochote

Kwa upande mwingine kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwadila amesema kuwa hatoi ahadi yoyote juu ya matarajio yake kwenye michuano hiyo.

Kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila akizungumza na wana habari hapo jana Juni 2 kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Kakamega Homeboyz leo (Picha-SPN)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Akijibu swali la mwandishi kutoka gazeti la Daily Nation la nchini hapa juu ya kutoonesha nia yoyote ya kutwaa ubingwa, Mwandila raia wa Zambia amesema si vyema kuanza kuahidi kwenye vyombo vya habari na badala yake shughuli yote itaonekana uwanjani.

“Hakuna sababu ya kutoa matarajio makubwa wakati hata mashindano hayajaanza na wala sipo hapa kwa ajili ya kuwafurahisha wana habari.

“Kama kuna makocha walikwambia kuwa watatwaa ubingwa wa Super Cup basi ni wao lakini mimi siwezi kusema hivyo.

“Najua kila kocha amekwambia hivyo lakini mashindano yakiisha utakuja kuniambia matokeo yake hivyo si kila anayesema atatwaa ubingwa hufanya hivyo, hivyo mimi najikita zaidi kwenye maandalizi ya timu yangu na si vinginevyo”, alikazia Mwandila wakati akimjibu mwandishi huyo.

Yanga na Kakamega watafungua pazia la michuano ya SportPesa Super Cup kwenye dimba la Afraha majira ya saa 7 kamili mchana huku mechi hiyo ikirushwa mubashara kupitia Star TV, Star Sports kupitia king’amuzi cha Continental sambamba na chaneli ya Sports Focus kupitia king’amuzi cha Star Times.


Spread the love

More in Habari