Connect with us

Habari

Singida Yatwaa Ushindi Wa Tatu Baada Ya Kuilaza Kakamega Kwa Penati 4-1

Spread the love

NAKURU, Kenya – Klabu ya Singida United imefanikiwa kuibuka washindi wa tatu wa michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuigaragaza Kakamega Homeboyz kutoka nchini Kenya kwa mikwaju ya penati 4-1

Ilibidi Singida wangoje changamoto ya mikwaju ya penati ili kuweza kuibuka washindi baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ambapo Singida walitoka nyuma na kusawazisha kupitia kwa Danny Lyanga dakika ya 61 kufuatia Kakamega kupata bao la uongozi kipindi cha kwanza lililofungwa na Wickleaff Opondo.

Ripoti Kamili

Singida walikuwa wa kwanza kufika langoni mwa Kakamega Homeboyz dakika ya kwanza ya mchezo baada ya wachezaji wa Kakamega kupoteza pasi eneo la hatari lakini hata hivyo shambulio hilo halikuweza kuleta madhara.

Haikuwachukua Kakamega muda mrefu kuandika bao la kuongoza ambapo dakika ya tatu tu ya mchezo, mshambuliaji Wickliffe Opondo aliandika bao la kwanza kwa shuti la karibu na lango lililomuacha golikipa Peter Manyika akiwa hana la kufanya.

Nusura Miraji Adam aiandikie Singida United bao la kusawazisha dakika mbili baadae, baada ya kuchonga krosi kutoka mashariki mwa uwanja iliyoenda moja kwa moja langoni na kugonga mwamba wa pembeni na kurudi uwanjani ukikosa mmaliziaji na kuishia kuokolewa vyema na wachezaji wa Kakamega.

Kakamega walionekana kuwa hatari zaidi huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa Singida ambao walikumbwa na kadhia ya kupoteza pasi mara kwa mara kwenye eneo la kiungo.

Dakika ya 35, golikipa Peter Manyika alitumia uzoefu wake vyema kuokoa mpira wa adhabu uliochongwa moja kwa moja langoni mwake huku Kakamega Homeboyz wakipoteza nafasi za kufunga mara kadhaa.

Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika, Kakamega walienda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa na mtaji wa bao moja.

Kipindi Cha Pili

Timu zote ziliendeleana kushambulia kwa zamu huku Singida wakifanya mabadiliko katika dakika ya 52 kwa kumtoa John Tibar na nafasi yake kuchukuliwa na Elinyesia Sumbi.

Dakika ya 61 Danny Lyanga aliiandikia Singida united bao la kusawazisha kwa kichwa cha kuchumpa baada ya kuchongewa krosi maridhawa kutoka winga ya kulia.

Kuingia kwa goli hilo kuliambatana na mabadiliko kwa upande wa Singida United ambapo nahodha Nizar Khalfani alimpisha mshambuliaji mpya raia wa Brazil, Felipe Santos.

Mabadiliko hayo yaliiibua Singida United kutoka kwenye usingizi mzito na kuanza kulishambulia lango la Kakamega Homeboyz kama nyuki.

Licha ya kushambuliana mara kwa mara, lakini si Singida United wala Kakamega Homeboyz aliyeweza kupata goli la pili hali iliyofanya mechi kwenda hatua ya matuta ambapo Kakamega walionekana kujiandaa mapema baada ya kocha Paul Nkata kumtoa golikipa Michael Wanyika na nafasi yake kuchukuliwa na mrundi McArthur Arakaza

Mikwaju ya Penati

Walikuwa ni Singida United walioibuka washindi wa tatu wa michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 4-1.

Penati za Singida ziliwekwa kimiani na Deus Kaseke, Miraji Adam, Shafiq Batambuze na Danny Lyanga huku golikipa Peter Manyika akifuta penati moja ya Kakamega Homeboyz huku nyingine mbili zikiota mbawa.

Kwa matokeo hayo sasa, Singida United wanajizolea kitita cha Dola 7,500 baada ya kuibuka washindi wa tatu wa mashindano haya ya mwaka huu huku nahodha Deus Kaseke akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi na jopo la makocha kutoka Everton waliopo uwanjani hapa.


Spread the love

More in Habari