Connect with us

Habari

Singida Yafuzu Nusu Fainali Ya Super Cup Baada Ya Kuichachafya Leopards Kwa Penati 4-2

Spread the love

NAKURU, Kenya -Klabu ya Singida United imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuitandika AFC Leopards kwa mikwaju ya penati 4-2.

Alikuwa ni golikipa Peter Manyika ambaye aliibuka shujaa ndani ya dakika 90 za mchezo baada ya kufanya kila lililowezekana kuizuia AFC Leopards kupata bao ikiwemo mkwaju wa penati aliouokoa dakika ya 70 ya mchezo na kumpa kocha Ally Suleiman Hemed ushindi wake wa kwanza akiwa kama kocha wa Singida United.

Ripoti Kamili

Singida ndio walikuwa wa kwanza kufika langoni mwa AFC Leopards ambapo mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji Mundia Lubinda uiishia kwenye mikono salama ya golikipa wa Leopards, Ezekiel Owade.

Hadi dakika 20 zinakatika, Singida walionekana kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa ingawa pasi ya mwisho ndio ilikosekana.

Dakika tatu baadae, Leopards walijibu mapigo baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Singida huku shuti la Brian Marita likipaa juu ya lango.

Ilibidi Peter Manyika afanye kazi ya ziada kuokoa mchomo uliochongwa na Jaffari Odenyi wa Leopards huku dakika mbili baadae Singida walikosa mabao mawili ya wazi baada ya washambuliaji wao Mundia Lubinda pamoja nae Danny Lyanga kukosa umakini ndani ya eneo la hatari la AFC Leopards.

Peter Manyika alisimama kidete kulitetea lango la Singida kwa mara nyingine baada ya kuruka kwa ustadi wa hali ya juu na kuokoa mpira uliopigwa na Ray Omondi huku dakika moja baadae akipangua tena mpira wa adhabu ulipigwa langoni mwake na nahodha wa leopards, Robinson Kamura

Golikipa wa Singida United Peter Manyika (jezi ya bluu) akiokoa moja ya hatari kwenye lango lake katika mchezo dhidi ya AFC Leopards ambapo Singida walishinda kwa mikwaju ya penati 4-2 (Picha – SPN)

Hadi mechi inakwenda mapumziko, si AFC Leopards wala Singida United aliyeweza kuliona lango la mwenzake katika mchezo uliokuwa wa vuta n’kuvute kwa pande zote mbili

Kipindi cha pili

Kipindi cha pili kilianza kwa masahibu langoni mwa Singida united ambapo ilimlazimu mlinda mlango Peter Manyika kuokoa michomo mitatu mfululizo iliyokuwa ikiingia kwenye nyavu zake na kuweza kuwanyima AFC Leopards bao la uongozi.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko ya hapa na pale ambapo Singida United kwa upande wao waliwatoa Elisha Muroiwa na Mundia Lubinda huku nafasi zao zikichukulia na Chuku Salum na Adam Miraji.

Nahodha wa Singida United Deus Kaseke (kushoto) akiwania mpira na machezaji wa AFC Leopards kwenye mchezo wa robo fainali ya SportPesa Super Cup (Picha – SPN)

Alikuwa ni shujaa Peter Manyika tena aliyeokoa mkwaju wa penati dakika ya 70 baada mlinzi wa Singida united kumfanyia madhambi Mchezaji wa AFC Leopards ndani ya eneo la hatari na kufanya matokeo kuwa 0-0.

AFC Leopards waliendelea kufanya mashambulizi ya hapa na pale langoni mwa Singida United lakini mashambulizi hayo hayakuweza kuzaa matunda na matokeo kubakia 0-0 hadi mwamuzi Eric Munirakiza alipopuliza filimbi ya mwisho kuashirikia kumalizika kwa dakika 90

Mikwaju ya Penati

Wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwenye robo fainali ya michuano hii hii iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwaka mmoja uliopita, Singida United waliweka kimiani mikwaju yao ya penati kupitia kwa Shafiq Batambuze, Miraji Adam, Danny Lyanga na Elinyesia Sumbi huku Kenny Ally akikosa penati ya kwanza kabisa.

Wachezaji wa Singida United wakiomba dua kuelekea kwenye changamoto ya mikwaju ya penati dhidi ya AFC Leopards ambapo walishinda kwa jumla ya penati 4-2 (Picha – SPN)

AFC Leopards wao walipata penati kupitia kwa Robinson Kamura na Whyvonne Isuza huku Baker Lukooya na Moses Mburu wakishindwa kutumbukiza kimiani penati zao

Kwa mantiki hiyo sasa, Singida United wanafuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup kwa jumla mikwaju ya penati 4-2 ambapo sasa watakutana na bingwa mtetezi, Gor Mahia Siku ya Alhamisi ya Juni 7.


Spread the love

More in Habari