Connect with us

Habari

Sam Vokes Atupia Mbili Huku Burnley Ikiizamisha Chelsea Darajani Kwa Mabao 3-2

Spread the love

LONDON, Uingereza -Mabingwa watetezi wa EPL, klabu ya Chelsea leo wameuanza msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Uingereza kwa kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Burnley kwenye dimba la Stamford Bridge jijini London.

Sam Vokes ndiye amekuwa nyota wa mchezo wa leo kwa upande wa Burnley baada ya kutupia magoli mawili kambani na kuwafanya vijana hao wa kocha Sean Dyche kuanza msimu mpya kwa kishindo cha aina yake.

Gundu lilianza mapema kwa Chelsea baada ya nahodha mpya wa mabingwa hao, Gary Cahill ambaye alimchezea rafu mbaya mchezaji wa Burnley huku mwamuzi Craig Pawson bila hiyana akimzawadia kadi nyekundu mnamo katika dakika ya 14 tangu mpira kuanza.

Baada ya kadi hiyo Chelsea walionekana kuzidiwa na Burnley katika umiliki wa mpira na dakika kumi baadae, mshambuliaji raia wa Wales, Sam Vokes aliiandikia Burnley bao la kuongoza akiunganisha vyema krosi iliyopigwa na Matthew Lowton kwa shuti la karibu lililopigwa kulia mwa goli na kumshinda golikipa Thibaut Courtois

Sam Vokes akishangilia baada ya kuifungia Burnley bao la kuongoza dhidi ya Chelsea. Picha/BurnleyOfficial -Twitter

Dakika ya 39, Stephen Ward aliandika bao la pili kwa upande wa Burnley kwa kichwa akiunganisha vyema krosi ya Jack Cork na kufanya matokeo kuwa 2-0 huku ikionekana kama Chelsea wamepoteaba uwanjani, Sam Vokes tena akaiandikia Burnley bao la tatu akimalizia vyema kazi ya Steven Defour mnamo dakika ya 43 ya mchezo na hadi mpira unakwenda mapumziko, matokeo yalikuwa 3-0

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Chelsea wakionekana kupata nguvu na dakika ya 59 ya mchezo, Alvaro Morata aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Michy Batshuayi ambaye hakuweza kuonesha cheche kwenye mchezo wa leo.

Dakika kumi tu tangu aingie, Morata aliiandiki Chelsea bao la kwanza kwa kichwa cha kuchumpa akimalizia vyema krosi ya Willian kutoka mashariki mwa uwanja goli ambalo liliwarudisha Chelsea mchezoni na kuanza kulisakama lango la Burnley kama nyuki.

Alvaro Morata akishagilia baada ya kuifungia Chelsea bao la kwanza. Picha /Chelsea FC -Twitter

Wakati Chelsea wakisaka magoli ya kusawazisha, Dakika ya 81 ya mchezo, Cesc Fabregas alilambwa kadi nyekundu na mwamuzi Craig Pawson baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Burnley na hivyo kuifanya Chelsea kucheza pungufu ikiwa na wachezaji tisa tu uwanjani.

David Luiz aliiandikia Chelsea bao la pili kwa shuti la chini chini akimalizia vyema pasi ya kichwa ya Alvaro Morata kufuatia mpira mrefu uliopigwa na Cesar Azpiliqueta.

Huenda Marcos Alonso angeweza kuwa shujaa kwenye mchezo wa leo baada ya kukosa goli sekunde ya mwisho ya mchezo kufuatia kazi nzuri ya uokoaji iliyofanywa na walinzi wa Burnley na hadi kipenga cha mwisho cha mwamuzi Craig Pawson kinapulizwa, ubao ulikuwa ukisomeka Chelsea 2 Burnley 3.

Kwa mantiki hiyo sasa, Chelsea itawakosa Gary Cahill na Cesc Fabregas kwenye mchezo unaofuata wa ligi dhidi ya Tottenham Hotspurs utakaopigwa Agosti 20 kwenye dimba la Wembley.


Spread the love

More in Habari