Connect with us

Habari

PSG VS Madrid: Ni Anguko La Unai Emery Na Neymar Au Ronaldo Na Zidane

Spread the love

PARIS, Ufaransa- Ulimwengu wa soka utashuhudia dakika nyingine 90 nzito kati ya miamba miwili ya soka barani Ulaya iliyosheheni wachezaji mahiri kwenye vikosi vyao.

Bado wengi wetu tunayakumbuka yale mabao mawili ya Cristiano Ronaldo na Marcelo kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza pale jijini Madrid ambapo PSG licha ya ubora wa kikosi chao, waliweza kukaa kwa mabao 3-1 dhidi ya bingwa mtetezi Real.

Baada ya wiki tatu za majuto ni mjukuu kupita, leo tunaenda kushuhudia mechi ya mwisho itakayoamua nani ataendelea na safari na nani atabwaga manyanga.

Huenda wengi wetu tumeumia kuona mechi kubwa kama hii ikipangwa kwenye hatua za awali za mtoano wakati tulikuwa na ndoto za kuwaona wakali hawa wakitoana jasho kwenye mechi ya fainali jijini Kiev, nchini Ukraine, Mei 26, 2018.

Hii ni mechi ambayo huenda ikaleta sura tofauti kwenye vikosi hivi viwili tishio baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Felix Brych kutoka Ujerumani kupulizwa pale dimbani Parc des Princes leo.

Anguko

Kwenye mechi hii ni lazima mmoja atoke na mmoja apite, ndio maana nathubutu kusema kuwa michuano hii itapoteza moja ya timu zenye uwezo wa kuchukua ubingwa tena katika hatua za mapema tu.

Real Madrid wakitolewa kwenye hatua hii itakuwa ni anguko kubwa sana kwao wakiwa kama mabingwa watetezi ambao bado walikuwa na uwezo wa kutetea taji lao na huenda safari ya Zinedine Zidane kwenye viunga vya Santiago Bernabeu ikaishia hapo.

Zinedine Zidane, Meneja Real Madrid

Zidane amekuwa na matokeo ya kusuasua msimu huu akiwa kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa LaLiga akiwa ameachwa na vinara Barcelona kwa tofauti ya alama 15 huku tetesi zikiwa zimezagaa kuwa anaweza kutimuliwa, hivyo matokeo ya mechi ya leo yakienda ndivyo sivyo basi safari yake itakuwa inaiva

Lakini pia litakuwa ni anguko kubwa kwa Unai Emery na PSG yake kama wakitolewa kwenye hatua hii hasa ukizingatia uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na matajiri wa klabu hiyo hususani kwenye usajiali.

Kuwa na mchezaji ghali zaidi duniani kama Neymar kwenye kikosi chako sambamba na Kylian Mbappe ni kigezo tosha cha kocha yoyote duniani kutwaa ubingwa wa UEFA na endapo PSG atatolewa kwenye hatua hii bila kujali katolewa na nani basi Unai Emery safari itakuwa inamhusu.

Ballon D’or

Hii ni mechi ambayo ina wachezaji wawili wenye uwezo wa kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa dunia maarufu kama Ballon D’or ambao ni Cristiano Ronaldo kwa upande wa Real Madrid na Neymar kwa upande wa PSG.

Kwa miaka mingi sasa michuano hii ya UEFA imekuwa na nafasi kubwa sana katika kuamua ni mchezaji yupi atatwaa tuzo hii, hivyo basi, kutolewa kwa Madrid au PSG kwenye hatua hii kunamaanisha mmoja kati ya Neymar au Ronaldo atakuwa ameiweka rehani nafasi yake ya kutwaa Ballon D’or huku kura pekee ikiwa imebaki kwenye kombe la dunia.

Unai Emery, Meneja wa PSG

Litakuwa ni jambo la kusikitisha kuona Ronaldo ambaye ametoka kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga angalau goli moja kwenye kila mechi ya UEFA hatua ya makundi akitolewa kwenye hatua hii ya 16 bora hali kadhalika kwa upande wa Neymar ambaye baada ya kusajiliwa kwa pesa za kufuru, kila mtu angetegemea kuona akiibeba PSG mabegani mwake na kuipa ubingwa wa kwanza wa UEFA licha ya tayari kukumbwa na jinazimi la majeruhi ambayo yatamfanya kuikosa mechi ya leo.

Hii ni mechi ambayo huenda tunaweza kusema imekuja mapema sana kwani kuna ladha fulani tutaweza kuikosa kuanzia hatua ya robo fainali kutoka kwa timu yoyote itakayoaga mashindano na ni vigumu sana kwa Unai Emery au Zinadine Zidane kukwepa panga baada ya matokeo ya mwisho ya leo.

Tukutane Parc des Princes!


Spread the love

More in Habari