Connect with us

Habari

Penati Ya Mwisho Ya Jonas Mkude Yaipeleka Simba Fainali Ya SportPesa Super Cup

Spread the love

NAKURU, Kenya – Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wamefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuichabanga Kakamega Homeboyz kwa mikwaju ya penati 5-4

Alikuwa ni Jonas Mkude aliyeandika penati ya tano nay a mwisho kwa upande wa Simba baada ya Kakamega kukosa penati yao ya tano iliyopaa juu ya lango na kujikatia tiketi ya kutinga fainali baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana

Ripoti Kamili

Mechi ilianza kwa kasi ndogo huku timu zote mbili zikisomana mbinu za kiuchezaji hivyo kushindwa kutengeneza nafasi za magoli.

Simba walionekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo ingawa pasi ya mwisho ilionekana kuwa tatizo kwa upande wao huku Kakamega nao wakitumia mipira mirefu kulikaribia lango la Simba ambazo hata hivyo hazikuonekana kuleta madhara.

Dakika ya 27, Kakamega walifanya shambulizi langoni mwa Simba ambapo hata hivyo shuti lao halikuweza kulenga lango.

Simba walianza kulisakama lango la Kakamega ambapo dakika ya 35, shuti la Shiza Kichuya lilishindwa kulenga lango la Kakamega na dakika mbili baadae, Haruna Niyonzima aliachia mkwaju ambao ulipanguliwa na golikipa wa Kakamega, Michael Gathoni na kuwa kona.

Hadi dakika 45 za mwamuzi Eric Munirakiza kutoka Burundi zinakamilka, hakuna timu iliyofanikiwa kuliona lango la mwenzake.

Kipindi cha Pili

Pamoja na mashabiki lukuki walioujaza Uwanja wa Afraha, nguli wa zamani wa klabu ya Everton na timu ya taifa ya Nigeria, Yakubu Aiyegbeni aliweza kujumuika na makocha watatu kutoka klabu ya Everton kwenye jukwaa kuu kuutazama mchezo huo.

Kipindi cha pili kilianza kwa mvutano wa hapa na pale lakini bado hakuna timu iliyoweza kupenya ngome ya timu pinzani na kuandika bao.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko ambapo Simba kwa upande wao walimtoa Juma Rashid na Rashid Mohamed na nafasi zao kuchukuliwa na Moses Kitandu pamoja nae Adam Salamba lakini hata hivyo bado Simba ilishindwa kufurukuta.

Licha ya Simba kupata faulo za hapa na pale zilizopigwa na Shiza Kichuya pamoja na Haruna Niyonzima lakini bado mipira hiyo ilikosa wamaliziaji huku ngome ya Kakamega ikionekana kuwa imara zaidi

Ilimlazimu mlinda mlango, Aishi Manula kufanya kazi ya ziada dakika ya 90 ya mchezo baada ya Kakamega kufanya shambulizi langoni mwa Simba ambapo Manula kwa ustadi wa hali ya juu aliudaka mpira wa kichwa uliokuwa ukielekea kujaa langoni mwake

Hadi dakika 90 zinamalizika, hakukuwa na timu iliyoweza kuliona lango la mwenzie hali iliyolazimu changamoto ya mikwaju ya penati kuingila kati ili kumpata mshindi atakayetinga hatua ya fainali.

Mikwaju ya Penati

Walikuwa ni wekundu wa Msimbazi walioibuka kidedea kwa mara nyingine tena baada ya kuibuka mashujaa kwa mikwaju ya penati 5-4 ambapo penati zao ziliwekwa kimiani na Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Shiza Kichuya na Jonas Mkude ambaye aliweka kimiani penati ya mwisho baada ya Kakamega Homeboyz kukosa penati ya tano.

Kwa hali hiyo sasa, Simba wanatinga fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup kwa jumla ya mikwaju ya penati 5-4 ambapo sasa watakutana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Gor Mahia na Singida United kwenye mechi ya fainali itakayopigwa siku ya Jumapili ya Juni 10 kwenye dimba la Afraha.


Spread the love

More in Habari