Connect with us

Habari

Okwi, Bocco Manula Wakizungumzia Thamani Ya Mchezaji Nje Ya Uwanja Kupitia Mitandao Ya Kijamii

Spread the love

DAR ES SALAAM, Tanzania- Kujiongezea thamani kama mchezaji limekuwa ni suala ambalo wanamichezo wengi hususani wa mpira wa miguu duniani kote wamekuwa wakilifanya katika kuhakikisha kuwa majina yao yanasimama kama nembo zinazokubalika na watu ndani na nje ya uwanja.

Wachezaji wa Simba Alhamisi ya wiki iliyopita walipata fursa ya kutembelea ofisi za SportPesa ambapo walipewa somo kuhusiana na jinsi ya kutengeneza nembo zao kupitia majina yao na moja ya njia za kuweza kufanya hivyo ni kupitia mitandao ya kijamii.

Baada ya kumalizika kwa somo hilo fupi na wachezaji kupata fursa ya kuuliza maswali mawili matatu, ilikuwa ni wakati muafaka kwa baadhi ya wachezaji kuweza kueleza walichokielewa kutokana na somo hilo ambalo kwao lilionekana kama ni kitu kipya.

Wakiongea na SportPesa News kwa nyakati tofauti, wachezaji wa Simba, Emmanuel Okwi, John Bocco na Aishi Manula walieleza kile walichokielewa kutoka kwenye somo hilo na kujitengeneza nembo (brand) zao kupitia majina yao kwenye mitandao ya kijamii na sehemu nyingine.

“Ni kitu ambacho nilikuwa najitahidi sana mimi kama mchezaji katika kujitengenezea nembo ya jina langu lakini kwa leo nimepata elimu na ni kitu ambacho nitakifanyia kazi zaidi ili niweze kupata kitu kutoka kwenye kipaji changu,” Emmanuel Okwi alisema.

Aishi Manula akichangia hoja juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii walipotembelea ofisi za SportPesa Oktoba 12 mwaka huu

“Ni kitu kizuri sio kwangu tu bali kwa wachezaji wote kwasababu ni vitu ambavyo tulikuwa hatuvijui hivyo kama kweli mtu una nia na unaelewa nini kilichosemwa basi ni fursa nzuri kwetu sisi wachezaji kuweza kujiendeleza nje ya uwanja,” John Bocco aliongeza.

Naye Aishi Manula akizungumzia matumizi ya kurasa zake za mitandao ya kijamii alikuwa na haya ya kusema: “Mwanzoni akaunti zangu za Instagram au Facebook nilikuwa nazichukulia kawaida tu sio kwamba nilikuwa nazichukulia kwa uzito mkubwa kama ambavyo tumesikia kwenye semina tuliyoipata. Kwa hiyo semina hii imetufungua macho tufikirie zaidi kwa ajili ya akaunti zetu tulizokuwa nazo,” alisema.

Wakati umefika

Bila shaka umefika muda muafaka kwa wachezaji wa mpira mguu kuweza kujitengenezea nembo zao kupitia majina yao kwenye mitandao ya kijamii na sehemu nyingine ili waweze kuongeza thamani zao kwa mashabiki na jamii inayowazunguka ili kuyatendea haki majina yao makubwa ambayo wameyajenga kupitia vipaji vyao.

“Nafikiri bado tunahitaji elimu kwasababu hatuwezi kusema tumefikia kwenye hatua kubwa kama wachezaji wenzetu wa Ulaya kwahiyo tunashukuru sana kama hivi tumepata elimu na tukiendelea kama hivi.

“Kujitengenezea nembo kupitia majina yetu ni kitu cha muhimu sana na sisi wachezaji inabidi tujiangalie katika vitu ambavyo tunaandika kwenye mitandao ya kijamii vinaendana na kazi yetu na visituangushe kwenye kazi yetu,” alisema Okwi.

Mtangazaji wa EATV, Salama Jabir akitoa somo kwa wachezaji wa Simba kuhusiana na matumizi ya mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi ya Oktoba 12

Naye John Bocco aliungana na hoja kwamba umefika muda muafaka kwa wachezaji wa kitanzania kujiweka kama wachezaji wa kulipwa na kuyatendea haki majina yao makubwa ambayo yanaweza kusimama kama nembo.

“Ni muda muafaka kwa sisi kujua, sio sisi tu wa Simba bali wachezaji wote Tanzania. Tuwashukuru SportPesa kwa kutupa darasa zuri kwa ajili ya maisha yetu ya baadae.”

Naye Aishi Manula alienda mbali zaidi na kudai kuwa; “Imefika muda kwa vile nilivyoelewa mimi hata picha tunazopiga tuwe na kamera zinazoeleweka na hata ikiwezekana kuwe na mchezaji ambaye anaweza kusimamia picha kabla hujaipost ili kuwafanya watu wapende kufuatilia akaunti yako.”


Spread the love

More in Habari