Connect with us

Habari

Mrithi Wa Mayanja Atambulishwa Rasmi Huku Manara Akichimba Mkwara Mzito

HATIMAYE klabu ya Simba imemtangaza kocha msaidizi mpya wa kikosi hicho, Djuma Masudi kutoka nchini Burundi ambaye amekuja kuziba nafasi ya Jackson Mayanja aliyeachi ngazi rasmi hapo jana.

Mapema asubuhi siku ya leo, SportPesa News iliripoti kuwa kocha huyo aliyeipa timu ya Rayon Sports ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliopita anatarajiwa kuwasili nchini leo ili kumalizana na klabu ya Simba na hatimaye kutangazwa rasmi.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye makao makuu ya klabu ya Simba yaliyopo mitaa ya Msimbazi-Kariakoo, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara alianza kwa kumkaribisha kocha huyo huku akimtahadharisha kuwa makini na vyombo vya habari.

“Naomba uwape ushirikiano wana habari lakini ushirikiano huo uende na tahadhari kwa sababu sisi watanzania ni waongo na tunapenda habari za kuzusha,” alisema Manara.

Nitakuwa mkali

Aidha Manara alionesha kusikitishwa kwake na taarifa za uzushi zinazoendelea kuzuka kuwa kocha Mkuu Joseph Omog naye ametuma barua kwenye uongozi wa Simba akitaka kujiuzulu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutolipwa mshahara wake.

“Natamani ningekuwa nafanya kazi kipindi kile cha zama za mawe ambapo kulikuwa hakuna mambo ya mitandao ya kijamii.

“Linapokuja suala la image (nembo) ya Simba nitakuwa mkali na naiomba serikali kuwachukulia hatua watu wanaozusha taarifa za uongo kwenye mitandao. Kwa taarifa hizi za uongo tutatengenezaje image ya klabu na hao wadhamini watakuja vipi sasa?” alihoji.

“Sisi Simba tatizo la kulipa mishahara halipo na haipiti tarehe 2 mishara haijalipwa.

Benchi jipya

Sambamba na kocha msaidizi mpya, Manara alimtambulisha meneja mpya wa klabu ya Simba, Richard Robert ambaye amechukua nafasi ya Dr Kapinga ambaye amerejea kwa muajili wake kuendelea na shughuli zake za uuguzi.

Robert ameshafanya kazi kama meneja wa viwanja vya ndege sambamba na Taasisi ya Jakaya Youth Park inayodhaminiwa na kampuni ya Symbion akiwa na taaluma ya masuala ya utawala na michezo.

More in Habari