Connect with us

Habari

Maoni Ya Mhariri: Nchi Za Afrika Mashariki Zitaweza Kuandaa AFCON Kama Zikiungana

KUANDAA MASHINDANO ya kimataifa ya soka limekuwa ni jambo gumu kwa nchi zetu za Afrika Mashariki ambazo kiwango cha soka kimekuwa ni cha kulenga kwa manati lakini pia suala zima la miundo mbinu na gharama kwa ujumla.

Hivi karibuni Kenya wamevuliwa uenyeji wa michuano ya CHAN ambayo inatarajiwa kufanyika mwakani kutokana na kusuasua kwa maandalizi ya miundo mbinu.

Rwanda wametutoa kimasomaso kwa kuandaa michuano ya AFCON ya U-17 mwaka 2011 sambamba na ile ya CHAN iliyofanyika mwaka jana wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa AFCON U-17 mwaka 2019.

Ni mwanzo mzuri kwa nchi zetu kuandaa michuano yenye uzito wa aina hii lakini je, tumeshawahi kufikiria kuandaa ile michuano mikubwa kabisa ya AFCON?

Sote tunajua kuwa ili nchi iweze kuandaa mashindano makubwa ni lazima bajeti kubwa itengwe ili kufanya marekebisho ya viwanja vyetu ambavyo sote tunafahamu ubovu wake, barabara, hoteli na miundo mbinu mingine ya msingi, lakini je, hali ikoje huku kwetu?

Mutwiri Mutuota, mwandishi mkongwe wa habari za michezo nchini Kenya na barani Afrika kwa ujumla ambaye ni mhariri mkuu wa SportPesa News Kenya ana haya ya kusema;

Hali halisi ilivyo

Ukiachana na Ethiopia, Nchi nyingine za Afrika Mashariki na kati zimekuwa na uhaba wa miundo mbinu ambayo itawawezesha kuandaa michuano mikubwa.

Kwa Kenya, kuna viwanja viwili ambavyo vinaweza kufaulu vigezo vinavyohitajika ambapo ni uwanja mmoja tu wa Moi International Sports Centre uliopo Kasarani ambao upo tayari kuandaa michuano ya kimataifa, ule mwingine wa Nyayo bado upo kwenye matengenezo.

Uwanja wa Moi International Sports Centre uliopo Kasarani jijini Nairobi

Nje ya Nairobi kuna miundo mbinu ambayo haiwezi kukidhi vigezo ikiwemo kukosekana kwa majukwaa ya kukalia n.k sawa na Uganda ambao wana uwanja wa Nakivubo pekee.

Kwa Tanzania kuna uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru ambapo viwanja hivyo vimepakana na nje ya Dar, kuna viwanja ambavyo  vinahitaji matengenezo makubwa.

Unahitaji angalau kuwa na viwanja sita vyenye hadhi sawa ili uweze kuandaa michuano ya kimataifa. Rwanda wameweza kuandaa michuano ya CHAN (ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya timu za taifa) mwaka jana ambapo uwekezaji wa hali ya juu ilibidi ufanyike, na ni wazi kuwa hawawezi kuingia gharama nyingine kubwa kuandaa AFCON hivi karibu.

Tunachotakiwa kufanya

Kinachohitajika kwa sasa ni nchi za Afrika Mashariki kutuma maombi ya kuandaa fainali kubwa za soka kama vile AFCON kwa pamoja.

Ili jambo hili liwezekane ni lazima tuwe na muunganiko wa miundo mbinu mizuri ya usafirishaji kwenye nchi zetu kama vile ndege maalum ili kuwezesha timu, vyombo vya habari na mashabiki kusafiri kutoka jiji moja kwenda jingine kwa haraka.

Tunaweza kuwa na kundi moja Nairobi, jingine Dar es Salaam, Kampala na Kigali na michuano ikifika i hatua ya mtoano, timu  na mashabiki wao wanasafiri kutoka jiji moja kwenda jingine kwa muda mfupi.

Mfumo huu sio mgeni kwasababu ni mfumo mpya wa mashindano ambao utaanza kutumika mwaka 2020 kwenye michuano ijayo ya mataifa ya Ulaya, (Euro 2020) ambapo majiji 13 kutoka nchi 13 tofauti yataandaa mashindano hayo kuanzia hatua ya makundi, 16 bora na robo fainali huku mechi za nusu fainali na fainali zitapigwa kwenye dimba la Wembley jijini London.

Uwanja wa taifa jijini Dar es salaam ukiwa kwenye matengenezo ya sehemu ya kuchezea kwa udhamini wa kampuni ya SportPesa

Faida zake

Mfumo huu sio tu kwamba utapunguza mzigo wa gharama za maandalizi kwa nchi moja, lakini pia utaongeza ushirikiano kwa nchi zetu za Afrika Mashariki sio tu kwa maneno lakini kwa vitendo kwani tayari tuna jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC ambapo suala kama hili litakuwa ni jambo rahisi endapo kama kila nchi itakuwa na dhamira ya dhati

UEFA wameamua kuanzisha mfumo huu wa mashindano wakiwa na kampeni yao ya Kuiunganisha Ulaya kupitia mpira wa miguu na kutoa fursa kwa nchi ndogo kisoka kama Arzebaijan kuonja radha ya kuandaa mashindano makubwa kama ya Euro na kuleta hamasa ya mpira kwenye nchi hizo.

Hiki ndicho Afrika Mashariki tunahitaji kwa sasa, hasa ukizingatia kuwa hakuna serikali yenye ubavu wa kutumia zaidi ya Sh Bilioni 88 kuandaa mashindano ya soka tu huku kukiwa na matatizo mengine ya kijamii yasiyohesabika.

AFCON inawezekana lakini je, Umoja wetu wa Afrika Mashariki upo tayari kuweka siasa pembeni na kujumuika kuandaa tukio moja la kimichezo la kihistoria ambalo litatuleta pamoja na kutangaza nchi zetu kimataifa?

More in Habari