Connect with us

Habari

Manula Aibuka Shujaa Simba Ikiifumua Kariobangi kwa Mikwaju ya Penati

Simba SC goal keeper, Aishi Manula, dives low to save Eric Juma's penalty for Kariobangi Sharks in their SportPesa Super Cup quarterfinal at Afraha Stadium, Nakuru on June 3, 2018. PHOTO/SPN
Spread the love

NAKURU, Kenya –Mabingwa wa Tanzania bara, Simba SC wamefanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuitandika Kariobangi Sharks ya nchini Kenya kwa mikwaju ya penati 3-2.

Golikipa Aishi Manula ndiye alikuwa nyota wa mchezo baada ya kupangua mikwaju miwili ya penati baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Afraha, wachezaji Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni na Jonas Mkude waliweka kimiani mikwaju ya penati kwa upande wa Simba huku Mohamed Hussein pamoja na Paul Bukaba wakikosa.

Ripoti Kamili

Simba waliuanza mchezo kwa kuonana vizuri ambapo walitumia muda mwingi kupiga pasi katika eneo la katikati mwa uwanja.

Tatizo la kupoteza mipira kwenye eneo la kiungo lilimfanya golikipa Aishi Manula kufanya kazi ya ziada baada ya kutoka nje ya eneo lake na kuokoa mpira kwa kichwa.

Dakika nane baadae Manula alilazimika kufanya kazi ya ziada baada ya mlinzi Yusuf Mlipili kushindwa kuokoa pasi ndefu iliyopigwa kuelekea langoni mwao

Mlinzi wa Simba, Shomari Kapombe akiwania mpira na mchezaji wa kariobangi Sharks kwenye mechi ya robo fainali ambapo Simba walishinda kwa mikwaju ya penati 3-2 (Picha -SPN)

Simba walisogea langoni mwa Kariobangi Sharks kwa mara ya kwanza ambapo shuti la Mohamed Ibrahim lilishindwa kulenga lango baada ya kupenyezewa pasi ya chini chini na Mohamed Hussein.

Kariobangi walifanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Simba ambapo pasi iliyopigwa kutoka winga ya kulia ilikosa mmaliziaji huku dakika tano baadae Simba walifanya mabadiliko kwa kumtoa Shomari Ally na nafasi yake kuchukuliwa na kinda Rashid Juma.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, si Simba wala Kariobangi Sharks aliyeweza kuchungulia nyavu za mwenzake.

Kipindi cha Pili

Simba walianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ambapo Marcel Kaheza aliingia kuchukua nafasi ya Mo Ibrahim lakini hata hivyo bado Simba ilishindwa kupenya ngome la Kariobangi.

Kukosa umakini kuliifanya Simba kupoteza mipira mara kwa mara hali iliyowaruhusu Kariobangi kufanya mashambulizi ya kushtukiza langoni mwao

Wachezaji wa Simba, Shiza Kichuya (mbele) na Jonas Mkude (katikati) wakingángána kumiliki mpira mbele ya mchezaji wa Kariobangi Sharks kwenye mechi ya robo fainali ya SportPesa Super Cup. (Picha – SPN)

Licha ya kumuingiza Shiza Kichuya, Moses Kitandu na Mzamiru Yassin ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Yusuf Mlipili aliyetolewa nje na machela baada ya kuumia, Simba walishindwa kupata bao hadi dakika 90 kadhalika Kariobangi Sharks na kufanya mechi kwenda kwenye changamoto ya mikwaju ya penati.

Mikwaju ya Penati

Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni na Jonas Mkude walipata penati kwa upande wa Simba huku Mohamed Hussein na Paul Bukaba wakikosa ambapo golikipa Manula aliibuka shujaa kwa kuokoa penati mbili za Kariobangi Sharks

Mchezaji wa Kariobangi Sharks akiwa amejiinamia kwa huzuni baada ya timu yake kupoteza mechi dhidi ya Simba kwa mikwaju ya penati 3-2 (Picha- SPN)

Na hivyo ndivyo wekundu wa msimbazi wameweza kutinga hatua ya nusu fainali kwa jumla ya mikwaju ya penati 3-2 ambapo sasa wanatarajiwa kukutana na Kakamega Homeboyz kwenye hatua ya nusu fainali siku ya Alhamisi ya Juni 7.


Spread the love

More in Habari