Connect with us

Habari

Mambo Matano (5) Ya Kuzingatia Kuelekea Fainali Ya Super Cup Kati Ya Gor na Simba

Spread the love

NAKURU, Kenya -Siku tisa za mshike mshike kwenye dimba la Afraha hatimaye zinafikia kikomo leo Juni 10 huku jasho la kutosha likiwa limemiminika bila kusahau sauti za mashabiki lukuki zilizowakauka makooni mwao.

Zilikuwa ni siku tisa zilizosheheni burudani ya kipekee kwa kila mpenda soka aliyebahatika kushuhudia kandanda la uhakika likisakatwa baina ya timu kongwe kutoka Afrika mashariki.

Baada ya kushuhudia upinzani wa hali ya juu huku kila timu ikitafuta nafasi ya kupenya katika raundi inayofuata, hatimaye ni mabingwa watetezi Gor Mahia na mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC wanaofanikiwa kukutana fainali.

Bila shaka ni mechi ambayo kila mtu angetamani kuona ikifunga mashindano haya kwa mwaka huu ili kuleta ladha halisi ya upinzani wa michuano hii baina ya vilabu kutoka nchi za Kenya na Tanzania.

Kwa kuzingatia hili, ebu tutazame baadhi ya mambo ya msingi kuelekea fainali hiyo ambayo itakuwa ya vuta n’kuvute.

Mabingwa Wa Ligi

Gor Mahia wanaingia kwenye fainali hii wakiwa kama mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya kadhalika wekundu wa Msimbazi ambao nao hivi punde wametoka kutawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Huenda fainali hii ikakata kiu na shauku ya wapenzi wa soka wanaotaka kujua Ligi ipi ni bora kati ya hizi mbili kwani kuwakutanisha mabingwa wa ligi hizo huenda ikawa ni kipimo sahihi.

Ingawa haitakuwa sahihi kusema ligi ipi ni bora kutokana na matokeo ya mechi moja lakini huwezi kuzuia hisia za mashabiki ambao wanaamini ubora wa Ligi hupimwa kwa jinsi bingwa wake anavyoweza kufurukuta pindi anapokutana na bingwa wa ligi nyingine.

Bila shaka tutakuwa na fainali nzuri iliyokidhi viwango hasa ukizingatia inawakutanisha mabingwa wa ligi mbili tofauti. Je, bingwa yupi atafurukuta? Tusubiri tuone.

Ngome imara

Achilia mbali ukubwa wa majina ya timu hizi, lakini namba nazo zinazidi kunogesha fainali hii.

Kama ulikuwa hujui, Simba na Gor Mahia ndio timu pekee ambazo hazijaruhusu bao lolote ndani ya dakika 90 tangu kuanza kwa michuano hii mwaka jana.

Gor Mahia imecheza mechi tano mpaka sasa kwenye michuano hii, tatu mwaka jana na mbili mwaka huu bila kuruhusu bao ikiwa imeshaweka kimiani jumla ya mabao 12 huku Simba kwa upande wao wakiwa hawajafunga goli lolote ndani ya dakika 90 lakini pia hawajaruhusu bao lolote katika mechi tatu walizocheza.

Takwimu hizi zinatuacha na maswali lukuki ambayo ni je, Simba itakuwa timu ya kwanza kutikisa nyavu za Gor Mahia ndani ya dakika 90 au Gor Mahia itakuwa timu ya kwanza kutikisa nyavu za Simba ndani ya dakika 90?

Lakini pia ukumbuke kuwa endapo Simba watapata bao kwenye mechi hii basi litakuwa ni bao lao la kwanza kwenye michuano ya SportPesa Super Cup. Je, mwisho wa siku namba zitatuambia nini?

Dylan Kerr VS Simba

Kivutio kingine kikubwa kwenye mechi hii ni kuwa Simba watacheza dhidi ya meneja wao wa zamani, Dylan Kerr.

Kerr aliachana na Simba Januari 2016 baada ya kuitumikia kwa takribani miezi sita tu kwa madai kuwa muingereza huyo ameshindwa kuifanya Simba kuwa timu ya kiushindani kama ilivyotarajiwa.

Kerr aliiacha Simba mikononi mwa kocha msaidizi Jackson Mayanja ikiwa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi nyuma ya Azam na Yanga.

Tangu Kerr atue Gor Mahia Julai mwaka jana, ameifanya timu hiyo kuwa miongoni mwa timu tishio Afrika Mashariki akiipokonya Tusker FC ubingwa wa Ligi ya Kenya sambamba na kuwapeleka wababe hao kwenye hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Ni wazi kuwa Kerr hawezi kusema hadharani kuwa ameipania Simba, lakini moyoni mwake anaujua ukweli na atataka kuudhihirishia umma kuwa Simba walikosea kumtimua miaka miwili iliyopita.

Simba bila Niyonzima

Simba itamkosa kiungo wake mahiri Haruna Niyonzima kwenye mchezo huu wa fainali baada ya mnyarwanda huyo kuoneshwa kadi mbili za njano kwenye michezo miwili iliyopita.

Niyonzima alioneshwa kadi ya njano kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Kariobangi Sharks pamoja na mchezo wa nusu fainali dhidi ya Kakamega hivyo kuukosa mchezo unaofuata kutokana na taratibu za kimashindano.

Najaribu kukifikiria kiungo cha Simba bila ya Niyonzima ambapo sasa ni Jonas Mkude na Mzamiru Yassin pekee waliosalia wakiwa kama wachezaji halisi wa nafasi hiyo.

Swali ni je, tutamshuhudia Kapombe akirudi kwenye kiungo cha kati kama alivyochezeshwa kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Kariobangi huku Shomari Ally akicheza kama mlinzi wa pembeni au Shiza Kichuya atarudi chini kidogo kusaidiana na kina Mkude?

Rekodi uso kwa uso

Mara ya mwisho Gor Mahia na Simba kukutana kwenye mechi ya kimashindano ilikuwa ni mwaka 1981 kwenye michuano ya vilabu bingwa Afrika Mashariki maarufu kama CECAFA.

Gor Mahia na Simba walipangwa kundi moja (B) sambamba na timu za KMKM kutoka Zanzibar na Breweries kutoka Uganda ambapo walitoka sare ya 0-0 kwenye mechi ya kwanza.

Gor wakiwa na wachezaji wao mahiri kama vile John Chore, Bobby Ogolla na Hamisi Shamba, waliongoza kundi wakiwa na alama 5 wakifuatiwa na Simba wenye alama 4 ambapo wawili hao walikutana tena kwenye mchezo wa fainali uliopigwa Februari 1.

Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa jijini Nairobi, K’Ogalo waliibuka na ushindi wa bao 1-0 ambapo Meya wa jiji la Nairobi kipindi hicho, Nathan Kahara aliwakabidhi nembo ya jiji la Nairobi kama ishara ya kuwapongeza.

Baada ya miaka 37 kupita, leo tutawashuhudia vigogo hawa wa soka Afrika Mashariki na Kati wakiumana kwa mara nyingine tena. Je, Gor kutamba tena kwenye ardhi ya nyumbani au Simba atasimika utawala mpya akiwa ugenini? Hakika dakika 90 hazitatuangusha.

Tukutane Afraha!


Spread the love

More in Habari