Connect with us

Habari

Makala: Ubora Wa City Unatukumbusha Ile Hadithi Ya “Nani Atamfunga Paka Kengele”

Spread the love

BILA SHAKA kwa wale ambao tulisoma St. Kayumba shule ya msingi tutakuwa tunaikumbuka ile hadithi mashuhuri kwenye kitabu cha somo la Kiswahili iliyokuwa ikijulikana kama “Nani atamfunga paka kengele.

Hadithi hii ilikuwa inamzungumzia paka aliyekuwa tishio kwenye kijiji walichokuwa wakiishi panya ambapo alishafanya maafa ya kutisha na kila kukicha si familia ya panya mabaka wala wenzie ambazo ziliachwa salama na paka huyu maarufu.

Baada ya kuishi kwa hofu, panya hawa waliamua kuita mkutano chini ya mti ambapo walipanga mikakati ya kukabiliana na paka huyu katili huku suluhisho pekee lilikuwa ni kumfunga paka huyo kengele ili atakapokuwa anakuja kengere inalia ili kila panya ajifiche kuinusuru nafsi yake, lakini suala likaja nani atamfunga paka huyo kengele?

Cha kusikitisha ni kuwa mti waliokuwa wamekaa, ndipo ambapo paka huyo alikuwa amejipumzisha kwa juu akiwasikiliza na alipotosheka na mazungumzo yao akaamua kushuka na kuwatafuna mmoja baada ya mwingine. Hakika ilikuwa ni hadithi ya kutisha na kusikitisha kwa wakati huo.

Kila nikifikiria jinsi Manchester City walivyo kwenye kiwango bora kwa sasa, siwezi kujizuia kuikumbuka hadithi hii ambayo baada ya kumaliza kusomwa na msichana mwenye sauti nzuri kuliko wote darasani, kila mmoja wetu alitoa mguno wenye chembe chembe za tanzia ndani yake.

Ubora

Pep Guardiola ndiye meneja ambaye ametumia hela nyingi kusaini wachezaji kwenye majira ya joto ambapo tuliona Ederson, Benardo Silva, Danilo, Banjamin Mendy, Gabriel Jesus na Kayle Walker na wengine wakitia saini zao.

Uongozi wa City haukuwa na mkono wa birika katika kufuata maagizo ya kocha wao ili kumpa anachotaka baada ya kukaa msimu mzima klabuni hapo bila ya kuwapa ubingwa wowote.

Pep Guardiola

Hakuna shaka kwamba City kwa sasa ni timu tishio sio tu nchini Uingereza bali hata barani Ulaya kutokana na aina ya wachezaji ilionao, mchezo inaocheza, na matokeo wanayopata.

City ina wachezaji mafundi ambao wanaweza kufanya chochote wakiwa popote na kikatimia na uzuri mwingine ni kuwa Guardiola wala haogopi kujilipua kwani anaweza kukupangia wachezaji saba kwenye kikosi chake cha kwanza ambao wana sifa ya ushambuliaji huku mkabaji akiwa ni mmoja au wawili tofauti na makocha wengine waoga ambao huamua kujilinda kwenye mechi kubwa.

Tumemuona City akiiadhibu Liverpool kwa mabao 5-0, akiirarua Watford 6-0, Craystal Palace 5-0 na hivi karibuni akiishushia Stoke City kipigo cha haja cha mabao 7-2 bila kusahau kipigo cha bao 1-0 walichokitoa darajani dhidi ya bingwa mtetezi, Chelsea.

Raheem Sterling, Gabriel Jesus, Sergio Aguero, Leroy Sane, Kevin De Bruyne ni wachezaji ambao wapo kwenye viwango bora kabisa kwa sasa wakipachika mabao wanavyotaka na kupiga pasi za hatari kadri wanavyojisikia.

Kevin de Bruyne akishangilia goli alilofunga kwenye mechi dhidi ya Chelsea, Stamford Bridge.

Kukutana na Man City wakiwa kwenye kiwango hiki ni hali inayoogopesha kama lile zoezi la kumfunga paka kengele lilivyokuwa.

City ya Guardiola inakushambulia muda wote na haipotezi mipira kizembe kwani kila mchezaji aliyepo uwanjani anaweza kumiliki mpira kuanzia kwa John Stones, kwenda kwa Fernandinho, David Silva, De Bruyne na hatimaye Aguero.

Takwimu

Mpaka kufikia sasa City wameshacheza mechi 12 za kimashindano msimu huu kwenye michuano mitatu ya EPL, Carabao Cup (Kombe la Ligi) na Ligi ya mabingwa Ulaya.

City wanaongoza EPL wakiwa na alama 22 kibindoni baada ya kucheza michezo nane wakiwa wamepoteza alama mbili tu kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Everton.

City imshaviadhibu vilabu saba ambavyo ni Brighton & Hove Albiol, Bournemouth, Liverpool, Watford, Crystal Palace, Chelsea na Stoke City huku wakifunga mabao 29 na kufungwa mabao manne tu

City hiyo hiyo inaongoza kundi F kwenye michuano ya ligi ya mabingwa ikiwa na alama tisa kibindoni baada ya kuvichakaza vilabu vya Shakhtar Donetski, Fayenoord na Napoli bila kusahau ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Brom kwenye kombe la Ligi.

Mpaka sasa City wameshapachika jumla ya mabao 37 na kuruhusu kufungwa mabao sita katika mechi 12 ikiwa ni wastani wa kufunga mabao matatu kila mechi na kuruhusu magoli 0.2 kila mechi.

Wachezaji wa City wakishangilia moja ya mabao katika ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya Stoke City mwishoni mwa wiki

Bado hatujawashuhudia wakicheza dhidi ya United, Arsenal, Spurs na vigogo wengine wa Ulaya kama PSG, Barcelona na wengine lakini tayari wameshaonekana kuwa ni aina ya timu ambayo ni tishio na inayoweza kupambana na yoyote yule na kupata matokeo.

Nathubutu kusema kuwa Man City ni timu iliyokomaa msimu uliopita kuliko misimu yote niliyowahi kuiona na imeshatuma salamu za onyo kwa vilabu barani Ulaya.

Hakuna anayetamani kukutana na City kwa sasa kama ambavyo hakuna anayetamani kubebeshwa jukumu la kumfunga paka kengele hasa baada ya kushuhudia maafa anayoyafanya bila huruma.

Nani atathubutu? Tusubiri tuone na Burnley ndiye anafuata jumamosi hii.


Spread the love

More in Habari