Connect with us

Habari

Makala: Kumruhusu Musonda Aende Ni Kuzalisha Kina De Bruyne Na Lukaku Wengine

Spread the love

MWANZONI mwa wiki, Instagram iliingia mdudu ambapo timbwili liliibuka kati ya kinda Charly Musonda na waajiri wake klabu ya Chelsea.

Musonda mwenye umri wa miaka 20, aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram akilalamika kitendo cha kutopewa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Chelsea na kocha Antonio Conte.

Mbelgiji huyo ana kipaji kikubwa kama ilivyo kwa wachezaji wengine waliowahi kupita Chelsea na wale ambao bado wapo ikiwa ni mazao ya academy ya klabu hiyo ambao ni mabingwa wa ligi Kuu ya Uingereza.

Musonda kama ilivyo kwa Mario Pasalic, Lewis Baker, Van Ginkel, Ruben Loftus Cheek, Nathan Chalobah, Gael Kakuta, Jeremy Boga na wengine wengi, amekuwa ni mhanga wa mikopo ya hapa na pale na pindi anaporudi klabu hapo basi benchi linamuita.

Sote tunatambua kuwa Chelsea ni klabu pekee duniani inayoongoza kwa kuwa na wachezaji wengi vijana ambao wapo kwa mkopo kwenye vilabu vingine.

Wachezaji hao zaidi ya 30 wamekuwa wakichezea vilabu vidogo ili kukuza viwango vyao wakisubiri bahati zao zifike ili siku moja waweze kuitumikia timu ya wakubwa ya Chelsea.

Kevin De Bruyne

Musonda ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa hilo halina ubishi na alidhihirisha hilo alilopewa nafasi kwenye mechi ya raundi ya nne ya Carabao Cup dhidi ya Nottingham Forest na kufanikiwa kufunga goli lake la kwanza klabuni.

Inaonekana wazi kuwa nyota huyo amechoka kuendelea kusugua mbao ndefu na hadi kuamua kuisuta Chelsea kunako Instagram hali ambayo imeibua tetesi kuwa kinda huyo anaweza kutolewa kwa mkopo mwezi Januari.

Kabla sijamkosoa Musonda, najaribu kuangalia wachezaji wa Chelsea waliofanikiwa kutoboa kupitia sera hiyo ya kununua vijana na kuwatoa kwa mkopo ambayo Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Michael Emenalo amekuwa ndio muumini mkubwa.

Thibaut Courtois na Andres Christensen ndio wachezaji pekee kwenye kikosi cha sasa cha Chelsea ambao wameweza kutoboa kupitia mfumo huo huku nyota kama vile Kevin De Bruyne, Romelu Lukaku, Nathan Chalobah, Nathan Ake, Domic Solanke na wengine wakishindwa kuvumilia na kuamua kuanza maisha mapya.

Romelu Lukaku

Kama Musonda ameanza kulalamika ni wazi kuwa na yeye yupo mbioni kubwaga manyanga kwasababu sioni jinsi ambavyo Antonio Conte anampa nafasi kwenye kikosi cha kwanza wakati kuna Eden Hazard, Willian Borges na Pedro ambao wanacheza nafasi yake.

Musonda akichoshwa na hali inavyoendelea ni wazi kuwa ataondoka na kwa kipaji chake kikubwa ni lazima atapata timu ambayo itamuendelea na atakuwa tishio huko mbeleni.

Tumemuona Kevin De Bruyne alivyokuwa mcharo huko Man City na ndio De Bruyne huyo huyo aliyewaliza Chelsea hivi majuzi tu bila kusahau jinsi Lukaku anavyotupia magoli huko Manchester United kama anavyotaka.

PhD Ya Uvumilivu

Sidhani kama wachezaji wanapaswa kulaumiwa kwa kuonekana kuchoshwa na mfumo huu lakini wachezaji hao wa Chelsea wanatakiwa waelewe kuwa ili kupata nafasi kwenye klabu kama Chelsea ni lazima uwe na kitu cha ziada.

Andres Christensen alisota sana hadi kufikia hatua ya kupata nafasi kikosi cha kwanza. Alienda Borussia Monchengladbag kwa mkopo akafanya mambo makubwa kiasi kwamba vilabu vikubwa kama Barcelona vilianza kumuhitaji na ndio hapo Antonio Conte alipomrudisha.

Andres Christensen

Thibaut Courtois alikaa Atletico Madrid kwa mkopo kwa misimu mitatu na akafanikiwa kuwa kipa machachari Ulaya akiwa na umri mdogo kiasi kwamba Mourinho akakubali kumtoa kafara mkongwe Petr Cech ili kuweza kumpa nafasi yeye.

Japo ni mara chache kutoboa katika mfumo huu lakini ni wazi inabidi uwe mvumilivu na ufanye kazi kwa bidii na ionekane ili uweze kupewa nafasi.

Kama Chelsea ikitumia hasira na kuamua kumuuza Musonda kwasababu ya alichokifanya basi bila shaka watakuwa wanajiandaa kuzalisha Kevin De Bruyne na Romelu Lukaku wengine ambao wataendelea kuwawinda ndotoni.


Spread the love

More in Habari