Connect with us

Habari

Hisia Za Hazard Na Conte Zinapotofautiana Kuelekea Mchezo Dhidi Ya Barca Leo

Spread the love

LONDON, Uingereza- Kwa mara ya 13 leo, Chelsea watakuwa wakicheza dhidi ya Barcelona kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Baada ya dunia kusimama kwa dakika 90 wiki iliyopita wakati Real Madrid ikiichabanga PSG, leo ni siku nyingine tena kushuhudia mechi nzito ambayo ndio huleta maana halisi ya mashindano haya kuitwa Ligi ya mabingwa.

Tunaingia kwenye mechi hii huku dunia nzima ikiitazama Chelsea kama timu inayoenda kupoteza kirahisi mbele ya Barcelona.

Huwezi kuzilaumu hisia za mashabiki hawa ambao licha ya baadhi yao kusukumwa na hisia, lakini hata takwimu pia zinawapa kibuli cha kufanya hivyo

Chelsea kwa sasa inajikongoja kuendelea kubaki Top 4 baada ya kukubali vipigo mfululizo kwenye EPL huku Barcelona yenyewe ikijivinjari kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na tofauti ya alama saba dhidi ya Atletico Madrid ambao wapo nafasi ya pili.

Hazard VS Conte

Huenda ikawa ni siku ya kuogofya kwa mashabiki wengi wa Chelsea ambao wamepoteza imani na timu yao, lakini bila shaka hakuna mtu anayeitamani mechi hii kwa mapana kama Eden Hazard.

Hazard amelithibitisha hilo kwenye mkutano na waandishi wa habari hapo jana dimbani Stamford Bidge maana ya kukiri kuwa anahitaji kucheza mechi nyingi zenye uzito huu ili aweze kuonesha uwezo wake kwenye anga za kimataifa.

“Ukitaka kuwa mchezaji bora duniani unahitaji kucheza mechi kubwa kama hizi na kesho (leo) ndio mechi na tunacheza mpira wa miguu kwa sababu ya mechi kama hizi,” alisema Hazard wakati akijibu swali la mwandishi wa habari aliyehoji juu ya utayari wa nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji kuelekea mchezo dhidi ya Barca

Nakubaliana na Hazard kwa asilimia zaidi ya 100 kuwa kwa upande wake ni moja ya mechi kubwa zitakazomuwezesha kuonesha ubora wake kwa kila mpenda soka duniani hususani akicheza dhidi ya mchezaji bora wa dunia mara tano, Lionel Messi.

Conte kwa upande wake hakuwa na jipya la kusema zaidi ya kuuaminisha umati wa wana habari kuwa yeye na kikosi chake wana shauku kubwa kuelekea mechi hiyo.

Muitaliano huyo anaamini kuwa mechi kama hii itamuwezesha kupima ubora na udhaifu wa kikosi chake na nini afanye ili kukiboresha zaidi huku akikiri kuwa watapata wakati mgumu pindi timu yake itakapokuwa haimiliki mpira kutokana na sifa ya Barcelona ya kumiliki mpira kwa muda mrefu.

Ukweli wa mambo

Binafsi nayaamini kwa asilimia zaidi ya mia moja maneno ya Eden Hazard aliyoawaambia waandishi wa habari kuwa ana furaha kucheza dhidi ya Lionel Messi kwa mara ya pili kwasababu kwa mchezaji wa kiwango chake anahitaji mechi kubwa kama hizi ili kudhihirisha ubora wake.

Hazard amekiri kuwa hajafikia ubora wa Messi au Ronaldo kama watu wanavyodai lakini amedai kuwa anahitaji mechi nyingi dhidi ya timu bora ili aweze kunoa makucha yake vyema.

Ungepata nafasi ya kutazama sura ya Hazard wakati akiongea na waandishi basi ungeweza kuona jinsi anavyoongea kwa shauku huku akimaanisha yale anayoyasema, lakini sio Conte.

Conte kama kocha hana Amani kabisa na huenda kama angepewa nafasi ya kuchagua timu ya kukutana nayo kwenye hatua hii basi angeweza kuichagua hata Besiktas.

Licha ya wachezaji wa Chelsea kufurahia mechi hii lakini Conte bado anahisi hajawa na kikosi imara cha kukutana na Barcelona kwa sasa hasa ukizingatia ubora wa kikosi chake msimu huu na aina ya matokeo anayopata.

Kuti Kavu

Conte amekuwa kwenye bifu zito na bodi ya Chelsea kutokana na kutosajiliwa kwa wachezaji anaowataka na tayari kumekuwa na uvumi kuwa huenda Luis Enrique akachukua nafasi yake msimu ujao.

Antonio Conte

Kwa hali ilivyo tete, hakuna kocha ambaye angetaka kukutana na Barcelona katika wakati huu ambao kwenye ligi yake ya nyumbani amefululiza mechi dhidi ya vigogo kama vile Manchester United na Man City halafu hapo hapo bado kuna mechi mbili dhidi ya Barca.

Mechi ya leo inaongeza ugumu wa mambo kwa Chelsea na ndio maana Conte anaonekana kabisa kutokuwa na amani huku akikwepa swali la mwandishi aliyehoji kama kocha huyo wa zamani wa Juventus ana kikosi imara cha kuikabili Barcelona.

Karata ya mwisho?

Huenda matokeo ya leo na ya kule Camp Nou wiki mbili zijazo yakarudisha morali ya Conte au yakaiua kabisa na hatimaye safari yake nchini Uingereza ikaishia hapo.

Bado Conte ana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mechi hii kwani ana faida moja kuu aliyobakiwa nayo dhidi ya mpinzani wake.

Chelsea inajua jinsi Barcelona inavyocheza na hadi wachezaji wao wa kikosi cha kwanza na wale wa akiba na hivyo ni rahisi kuwaandalia mkakati wa kuwazuia, lakini sina uhakika kama Ernesto Valvede anajua jinsi Chelsea inavyocheza.

Wachezaji wa Chelsea wakishangilia moja ya magoli

Chelsea imekuwa ikibadilika kila mechi kuanzia kwenye mfumo hadi wachezaji wanaoanza na imekuwa ni ngumu kujua kama Chelsea inatumia mipira mirefu au pasi fupi fupi, inatumia mawinga kutengeneza nafasi au viungo wa kati.

Huenda hiyo ikawa ni faida kwa Conte kwani mpaka sasa nina uhakika ni yeye na benchi lake la ufundi pekee ndio wanajua watatumia mfumo gani na mchezaji gani ataanza, huku ikiwa ni tofauti kwa upande wa pili kwani hata mtoto wa miaka nane anaweza kukupangia kikosi cha Barcelona kitakachoanza leo.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, Conte amekuwa akijaribu mifumo tofauti tofauti kwa wachezaji mbalimbali kila mechi ila kujaribu kupata suluhisho la matatizo ya kikosi chake tofauti na Barca ambao wana kikosi chao cha ushindi kinachojulikana ambacho huanza kila mechi.

Hivyo sio ajabu katika jaribu jaribu za Conte, mfumo wa leo ukakubali na akaishangaza dunia na usisahau ni kipigo kutoka kwa Arsenal ndicho kiliibadili Chelsea na kuwawezesha kutwaa ubingwa wa EPL msimu uliopita.

Tukutane darajani!


Spread the love

More in Habari