Connect with us

Ligi Kuu ya Uingereza

Haya Ndiyo Maswali Magumu Matano (5) Ya Kujiuliza Kuelekea Mechi Kati Ya Chelsea na Burnley Leo.

Spread the love

LONDON, Uingereza – Mabingwa watetezi Chelsea watalifungua pazia la EPL leo watakapowaalika Burnley kwenye dimba la Stamford Bridge majira ya saa 11 jioni.

Chelsea wanaingia uwanjani huku macho na masikio yote yakielekezwa dimbani hapo kuona kama kocha Antonio Conte atakuwa na jambo jipya atakalokuja nalo

Chelsea kama vilabu vingine, wamefanya usajili ambapo wamewachukua Alvaro Morata kutoka Real Madrid, Tiemoue Bakayoko kutoka Monaco, Antonio Rudiger kutoka Roma na golikipa Willy Caballero kutoka Manchester City.

The Blues hawajawa na matokeo mazuri kwenye msimu wa maandalizi ambapo wamepoteza mechi kadhaa huku pia wakilipoteza kombe la ngao ya hisani dhidi ya Arsenal Jumapili iliyopita kwenye dimba la Wembley.

Antonio Conte amekuwa akikaririwa na vyombo vya habari mara kadhaa akiilalamikia bodi ya Chelsea huku akikerwa na kitendo cha yeye kutokuwa na nguvu ya kuamua wachezaji wa kusajili.

Chelsea wamemuuza Nemanja Matic na mpaka sasa hawajapata mrithi wake huku pia Conte akiendelea kusisitiza suala la kuwa na mawinga wakabaji ili kutoa changamoto kwa Victor Moses na Marcos Alonso ambao wanaonekana kutokuwa kati kiwango chao cha kawaida.

Chelsea wataingia uwanjani leo bila ya Victor Moses ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu huku pia wakimkosa kiungo mpya Tiemoue Bakayoko ambaye ana majeraha sambamba na Pedro na Eden Hazard ambapo pia watakosekana.

Kutokana na kukosekana kwa wachezaji hao, Antonio Conte anabakiwa na machaguo machache ya wachezaji kwenye kikosi chake cha kwanza ambapo huenda akafanya mabadiliko mchache ambayo yanaweza kuwashangaza wengi.

Haya ndiyo maswali magumu ya kujiuliza kabla hatujajua kikosi cha kwanza cha Chelsea leo.

Charly Musonda ataanza?

Huenda tukamuona kinda Charlie Musonda akianza kwenye kikosi cha kwanza leo kutokana na ukweli kuwa Conte anakumbwa na uhaba wa mawinga washambuliaji ambapo leo sio Hazard wala Pedro watakuwepo.

Charly Musonda

Endapo kama Conte atachezesha mfumo wa 3-4-3 ina maana watu watatu wa mbele ni mshambuliaji mmoja na mawinga wawili, na winga pekee ambaye yupo vizuri kucheza ni Willian hivyo endapo kama Conte akichezesha mfumo wake wa kawaida basi tujiandae kumuona Musonda ambaye alionesha kiwango kizuri kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Inter Milan akianza.

 Morata ataanzia wapi?

Katika mechi kadhaa ambazo Morata amecheza kwenye kikosi cha Chelsea mpaka sasa, mara nyingi amekuwa akianza kama mshambuliaji wa pembeni kwenye mfumo wa 3-4-3 huku Michy Batshuayi ambaye amefunga mabao 5 kwenye mechi za maandalizi akianza kama mshambuliaji wa kati.

Alvaro Morata

Sote tunaujua uwezo wa Morata akianza katikati lakini mpaka sasa ameshindwa kuonesha makali yake huenda kutokana na nafasi anayopangwa.

Conte anaweza kufanya maamuzi magumu ya kuendelea kumuanzisha Morata pembeni au akajitosa kumuanzisha mshambuliaji huyo katikati huku tukimshuhudia Michy Batshuayi akianzia benchi kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Conte ataendelea kumuamini Batshuayi?

Michy Batshuayi amekuwa na kiwango bora kwenye msimu wa maandalizi ambapo ameweza kufunga magoli matano katika mechi nne.

Michy Batshuayi

Kutokuwepo kwa Diego Costa ni wazi kuwa Conte amekuwa na ufinyu wa washambuliaji na hata baada ya ujio wa Morata bado Conte ameendelea kumuanzisha Batshuayi katikati.

Leo Conte hatakuwa na baadhi ya mawinga washambuliaji hivyo huenda akalazimika kuanzisha washambuliaji wawili.

Kama ataanza na washambuliaji wawili wote basi swali la kujiuliza ni kuwa ataendelea kumuanzisha Batshuayi kama mshambuliaji wa kati na kama ataanzisha mshambuliaji mmoja mbele, huyo mshambuliaji atakuwa ni Batshuayi?

Conte atahamia 3-5-2?

Kutokana na uhaba wa mawinga huku akiwa na washambuliaji wawili, usishangae kuona Conte akirudi kwenye mfumo wake pendwa wa 3-5-2 ambao bado hajaanza kuutumia Chelsea.

Antonio Conte

Huenda akafikia maamuzi hayo baada ya kuwa na Morata na Batshuayi mbele kwa kuhofia kumpanga mmoja wao pembeni hiyo akaamua kuwaanzisha wote wawili na pengine huo ndio ukawa mfumo sahihi kutokana na aina ya wachezaji alionao leo.

Willian atacheza wapi?

Ukiachana na Jeremy Boga na Charlie Musonda, Willian ndie winga pekee mzoefu aliyepo kwenye kikosi cha leo hivyo ni lazima tumuone akianza hasa baada ya Hazard na Pedro kutokuwa fiti.

Willian

Endapo kama Conte atachezesha 3-4-3 basi ni jibu jepesi kuwa Willian atacheza kama winga mshambuliaji kwenye safu ya watu watatu wa mbele, lakini endapo kama Conte atachezesha 3-5-2 basi ni wazi kuwa Willian atapata majukumu mapya.

Safu ya kiungo ya mfumo wa 3-5-2 ina wachezaji watano ambao ni mawinga wakabaji wawili wa pembeni, (Azpiliqueta na Alonso), viungo wa kati wawili (double pivotal) ambao ni Fabregas na Kante huku Willian akitafutiwa sehemu ya kuwekwa.

Hataweza kucheza pembeni kwasababu yupo Alonso na Azpiliqueta na hawezi kucheza katikati ya Fabregas na Kante hivyo ni suala lililo wazi kuwa atacheza mbele ya viungo wawili wa kati huku pia akiwa nyuma ya washambuliaji wawili wa mbele.

Willian anaweza kuwa mtu muhimu zaidi leo kwasababu kama Conte akimuanzisha Batshuayi na Morata mbele basi ni wazi kuwa lazima Willian acheze nyuma yao ili kuwalisha lakini pia wakati huo huo atakuwa na jukumu la kusaidia safu ya kiungo inayoongozwa na Fabregas na Kante ili isipwaye hususani pale wanapokuwa wanashambuliwa.

Hii ni mechi yenye mtego sana kwa Antonio Conte kwani atakuwa anajishauri kama amwanzishe Morata pembeni huku akijua fika tangu aanze kufanya hivyo hajawahi kupata ubora wa Morata huku pia akijishauri endapo kama amuanzishe Batshuayi  katikati kutokana na ubora aliouonesha siku za hivi karibuni.

Ni kitendo cha kusubiri na kuona jinsi Conte atakavyokuja na muarobaini wa mechi ya leo.


Spread the love

More in Ligi Kuu ya Uingereza