Connect with us

Habari

Haya Ndiyo Mambo Sita (6) Yaliyojiri Kwenye Hatua Ya Robo Fainali SportPesa Super Cup

Spread the love

NAKURU, Kenya -Hatua ya robo fainali ya mashindano ya SportPesa Super Cup imemalizika hapo jana huku wapo walionuna na pia wapo waliocheka.

Hatua hiyo ya kwanza inakamilika kwa timu za Yanga na JKU kutoka Tanzania sambamba na Kariobangi Sharks na AFC Leopards kutoka Kenya kufungashwa virago.

Safari ya kwenda Goodison Park kucheza na Everton inabaki kuwa ya Kakamega Homeboyz na Gor Mahia kwa upande wa Kenya pamoja nazo Simba na Singida United kutoka Tanzania ambazo zitatoana jasho kwenye nusu fainali kuwania nafasi mbili za fainali.

Hakika siku tatu za mwanzo kwenye mashindano ya mwaka huu zimekuwa na msisimko wa hali ya juu huku tukiweza kushuhudia mambo mengi yenye kufurahisha na kustaajabisha.

Kwa kulizingatia hilo, ebu tujikumbushe mambo sita (6) yaliyojitokeza ambayo huenda mengine uliyasikia au kuyaona lakini hukuweza kutilia maanani kwa wakati huo au hukusikia au kuyaona kabisa.

Penati 3 Ndani Ya Dakika 90

Kwenye kila mechi ya robo fainali kumepatikana penati ndani ya dakika 90 kasoro mechi moja tu ya Simba na Kariobangi.

SpotPesa Super Cup: Spot On Singida Break Leopards Hearts

Kipa wa Singida United, Peter Manyika akipangua penati kwenye dakika ya 70 ya mchezo dhidi ya AFC Leopards. Picha – SPN)

Katika penati zote hizo tatu, ni penati ya Allan Wanga pekee dhidi ya Yanga kwenye mechi ya ufunguzi ambayo iliweza kuzama kimiani lakini Gor Mahia na AFC Leopards walishindwa kufunga penati zao dhidi ya JKU na Singida United baada ya magolikipa Mohamed Mohamed (JKU) na Peter Manyika (Singida United) kufanya kazi ya ziada.

Je, huu ni uzembe wa wapigaji au umahiri wa magolikipa?

Dakika 12 Za Marcel Kaheza

Kwenye mechi dhidi ya kariobangi Sharks, kocha wa Simba Pierre Lechantre alimtoa Mohamed Ibrahim mwanzoni mwa kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji aliyesajiliwa hivi karibuni, Marcel Kaheza ambae dakika 12 baadae, alimtoa tena na nafasi yake kuchukuliwa na Shiza Kichuya.

Kwa hesabu za haraka haraka Kaheza alicheza dakika 12 tu japo sina uhakika sana alifanikiwa kugusa mpira mara ngapi kwenye hizo dakika 12 alizokanyaga nyasi za dimba la Afraha.

Sio mara ya kwanza kwa jambo kama hili kutokea kwenye soka lakini ni mara ya kwanza kutokea kwenye michuano ya SportPesa Super Cup na hata wale mashabiki wa Simba waliokuwa wamekaa mkao wa kula kumuona mchezaji wao huyo mpya hawakuweza kumfaidi ipasavyo.

Gubu la Lechantre

Kama ulifanikiwa kuutazama mchezo wa Simba dhidi ya Kariobangi kwa umakini mkubwa utagundua kocha wa Simba, Pierre Lechantre alikuwa hatulii kitini.

Haipiti dakika moja kocha huyo Mfaransa hajanyanyuka kama sio kumlalamikia mwamuzi wa mezani basi ataliamsha kwa mwamuzi wa pembeni.

Kocha wa Simba, Pierre Lechantre akitoa maelekezo kwa wachezaji wake kwenye mchezo dhidi ya Kariobangi Sharks (Picha – SPN)

Burudani zaidi ilikuwa ni pale Lechantre alipohisi maamuzi ya refa sio sahihi hivyo alikuwa akimsubiri mwamuzi wa pembeni asogee karibu na eneo lake la benchi ili amseme na kumlalamikia na alifanya hivyo kila mshika kibendera yule aliposogea karibu yake.

Hakika ilikuwa ni burudani kutazama vuta n’kuvute ile kati ya kocha na mwamuzi wa pembeni na ni busara tu za mwamuzi wa kati zilizomfanya Lechantre kuendelea kubaki kwenye benchi lasivyo kocha huyo angemaliza mechi akiwa jukwaani.

Kero Za Manyika Na Manula

Mpaka sasa naweza kusema Aishi Manula na Peter Manyika ndio magolikipa bora wa mshindano.

Magolikipa hawa wameweza kuzibeba Simba na Singida United migongoni mwao na kuzipelekea kwenye hatua ya nusu fainali kutokana na umahiri wao mkubwa.

Golikipa wa SImba, Aishi Manula akipangua moja ya penati kwenye mechi dhidi ya Kariobangi Sharks (Picha – SPN)

Utamkumbuka Manula jinsi alivyofuta penati mbili za wachezaji wa Kariobangi Sharks huku ndani ya dakika 90 akiuweka mwili wake rehani ili kuokoa michomo ya hapa na pale.

Sahau kuhusu Manula kwani huyo Manyika ndio alikuwa hafai. Achana na ile penati aliyochomoa dakika ya 70 lakini ile mikwaju mitatu aliyoitoa mfululizo mwanzoni mwa kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya Leopards.

Mara ya mwisho kuona umahiri wa namna ile ilikuwa ni mechi ya Chelsea na Sunderland mwaka jana ambapo Thibaut Courtois alifanya kufuru ile bila kumsahau Petr Cech ambaye alikuwa kikwazo kweye fainali ya UEFA kati ya Chelsea na Manchester United jijini Moscow mwaka 2008.

Ilifika kipindi mashabiki wa Leopards waliokuwa jukwaani walifura kwa hasira baada ya kuona jinsi Manyika anavyowanyima magoli ya wazi. Hakika walikereka!

Singida Yalipa Kisasi

Kama una kumbukumbu nzuri, Singida United walikutana na AFC Leopards kwenye hatua hii hii ya robo fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup Uwanja wa Uhuru ambapo Leopards walishinda kwa mikwaju ya penati.

Wachezaji wa Singida United wakishangilia baada ya kushinda kwa mikwaju ya penati 4-2 dhidi ya AFC Leopards hapo jana (Picha – SPN)

Ushindi wa jana wa Singida United kwa mikwaju ya penati 4-2 dhidi ya Leopards ni sawa na kulipa kisasi kwa kile kilichotokea msimu uliopita.

Singida wametuthibitishia kuwa malipo ni hapa hapa duniani.

Derby Mbili Kubwa Zimeepukwa

Endapo kama Yanga wangemfunga Kakamega Homeboyz na kutinga nusu fainali basi wangeweza kukutana na Simba; lakini Kakamega akaona isiwe shida, akamtoa Yanga hivyo kwa namna hiyo tumeikosa mechi ya Simba na Yanga kwenye nusu fainali.

Wachezaji wa Kakamega wakishangili moja ya mabao yaliyofungwa na Allan Wanga kwenye mechi dhidi ya Yanga (Picha – SPN)

Lakini pia Singida United nae akaona isiwe tabu, akamfungasha virago AFC Leopards na hivyo kumzuia kukutana na hasimu wake mkubwa, Gor Mahia kwenye hatua ya nusu fainali.

Huenda tungeweza kushuhudia derby mbili kubwa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati zikirindima kwenye dimba la Afraha lakini ‘’Roho mbaya’’ za Singida United na Kakamega zimeharibu mambo. Mwisho wa siku timu bora ndio zimeshinda!

Leo tupo mapumziko kidogo huku tukisubiri nusu fainali mbili za kesho ambapo Kakamega Homeboyz wanaumana na Simba kwenye mechi ya kwanza itakayopigwa majira ya saba kamili mchana huku Gor Mahia na Singida United wakitunishiana misuli kwenye nusu fainali ya pili itakayoanza majira ya saa tisa na robo mchana.

Tusubiri tuone timu zipi zitakata tiketi kucheza fainali siku ya Jumapili ili kumpata bingwa mmoja atakayeenda nchini Uingereza kucheza na Everton kwenye dimba la Goodison Park.


Spread the love

More in Habari