Connect with us

Habari

Gor Mahia Yatinga Nusu Fainali Ya Super Cup Baada Ya Kuitungua JKU 3-0

Gor Mahia FC players celebrate the opening goal against Jeshi la Kujenga Uchumi from Zanzibar during their quarterfinal clash at Afraha Stadium Nakuru on Sunday, June 3, 2018. PHOTO/SPN
Spread the love

NAKURU, Kenya – Mabingwa watetezi wa michuano ya SportPesa Super Cup, Gor Mahia, wameanza vyema kutetea ubingwa wao baada ya kuitandika JKU kutoka visiwani Zanzibar kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa robo fainali.

Mabao kutoka kwa George Odhiambo, Godfrey Walusimbi na Meddie Kagere yalitosha kabisa kulizamisha jahazi la mabingwa hao wa Tanzania visiwani na kuendeleza wimbi la ushindi kwenye michuano hiyo inayofanyika kwa mwaka wa pili mfululizo

Mechi ilianza kwa kasi ya kawaida huku timu zote mbili zikipiga pasi fupi fupi na kushambulia kwa kushtukiza ingawa JKU ndio walikuwa wa kwanza kufika langoni mwa Gor Mahia lakini hata hivyo pasi mujarabu iliyopigwa kutoka magharibi mwa lango la Gor ilikosa mmaliziaji kwa upande wa JKU

Timu zote mbili ziliendelea kushambuliana kwa zamu na kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo Gor Mahia walianza kuutawala mchezo kidogo kidogo.

Gor Mahia walipata penati dakika ya 22 ya mchezo baada ya mlinzi Suleiman Mwinjuma kumchezea madhambi mchezaji wa Gor Mahia ndani ya eneo la hatari ambapo hata hivyo nyanda wa JKU, Mohamed Mohamed alipangua penati hiyo kwa ustadi wa hali ya juu.

K ’Ogalo waliendelea kulisakama lango la JKU kama nyuki ambapo dakika nane baadae alikuwa ni George Odhiambo maarufu kama Blackberry aliyeipatia Gor Mahia bao la kuongoza baada ya kumzidi maarifa mlinzi wa JKU na kuweka mpira kambani mita chache akiwa na golikipa.

Huku mashabiki walioujaza uwanja wa Afraha wakizizima kwa nyimbo za kutia moyo kwa wachezaji wao, alikuwa ni Godfrey Walusimbi aliyepachika bao la pili kwa upande wa Gor Mahia dakika ya 35 akifumua shuti la chini chini ambalo lilimuacha mlinda mlango wa JKU, Mohamed Mohamed akigaa gaa chini bila mafanikio.

Kuingia kwa goli hilo kuliifanya Gor Mahia kulishambulia goli la JKU huku wakipigiana pasi fupi fupi zenye macho katika eneo la katikati ambalo lilionekana kumilikiwa na kiungo wa Gor Mahia na timu ya taifa ya Kenya, Francis Kahata na hadi mechi inakwenda mapumziko, mabingwa watetezi Gor Mahia walikuwa mbele kwa mabao 2-0

Kipindi cha pili mambo hayakubadilika sana kwani ni Gor Mahia walioendelea kutawala na kuwapa JKU wakati mgumu huku kukiwa na kosa kosa za hapa na pale.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko ambapo mshambuliaji Meddie Kagere aliyetokea benchi aliiandikia Gor Mahia bao la tatu kwa kichwa cha kuchumpa akiunganisha krosi mujarabu kutoka winga ya kulia ambayo ilishindwa kuokolewa kwa wakati na walinzi wa JKU na hadi dakika 90 zinamalizika, Gor mahia walikuwa mbele kwa mabao 4-0

Gor Mahia wanakuwa timu ya pili kufuzu kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup wakifuata nyayo za Kakamega Homeboyz ambao wamewatoa Yanga kwenye mechi ya mapema na kuendeleza rekodi ya kutoruhusu bao hata moja kwenye michuano hii ambayo ilianzishwa mwaka jana.


Spread the love

More in Habari