Connect with us

Habari

Gor Mahia Yatinga Fainali Ya Super Cup Baada Ya Kuilaza Singida Kwa Mabao 2-0

Spread the love

NAKURU, Kenya –Mabingwa watetezi wa michuano ya SportPesa Super Cup, timu ya Gor Mahia, wamefanikiwa kutinga hatua ya fainali baada ya kuichabanga Singida United kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili.

Mabao mawili ya Meddie Kagere moja kipindi cha kwanza na jingine lililofungwa kipindi cha pili yalitosha kusimika utawala wa Gor Mahia kwenye michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka jana ambapo mpaka sasa mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kenya hawajaruhusu goli hata moja tangu kuanza kwa michuano hii mwezi Juni mwaka jana.

Ripoti Kamili

Gor Mahia waliuanza mchezo kwa kuleta shinikizo kubwa langoni mwa Singida United ambao walionekana kuhimili mashambulizi ya mabingwa hao watetezi.

Dakika ya 9, Meddie Kagere alishindwa kuiandikia Gor Mahia bao la kuongoza baada ya kukosa utulivu langoni licha ya kumzidi ujanja mlinzi wa Singida na kujikuta shuti lake likipaa juu ya lango.

Dakika moja baadae, mlinda mlango Peter Manyika alifanya kazi nzuri kuzuia mpira wa krosi uliokuwa ukitafuta mmaliziaji langoni pake na kufanya matokeo kubaki 0-0.

Mvua ilianza kushuka kwenye mji wa Nakuru ambapo Singia United walilikaribia lango la Gor Mahia lakini hata hivyo shuti la nahodha Deus Kaseke lilishindwa kulenga lango sawa sawa

Dakika ya 34 nusura Deus Kaseke aiandikie Singida United bao la kuongoza baada ya kupiga shuti lililomshinda mlinda mlango Shaaban Odhoji na kugonga mwamba wa juu.

Gor Mahia walijibu mapigo dakika moja baadae ambapo mshambuliaji Meddie Kagere alifanikiwa kuvunja ngome ya Singida United na kuandika bao la kuongoza kwa kichwa cha kuchumpa kufuatia mpira wa kona uliojazwa langoni mwa Singida kushindwa kuokolewa kwa wakati.

Hadi mwamuzi Nsoro Ruzindana kutoka Rwanda anapuliza filimbi kuashiria kumalizika kwa kipindi cha kwanza, Gor Mahia walitoka kifua mbele kwa uongozi wa bao 1-0.

Kipindi cha Pili

Ni Gor Mahia walioendelea kulishambulia lango la Singida United kwa kasi licha ya uwanja kujaa maji hali iliyofanya wachezaji kuteleza mara kwa mara.

Dakika ya 61, Singida United walifanya shambulizi kwenye lango la Gor Mahia lakini mpira wa kichwa wa Mundia Lubinda ulishindwa kulenga lango baada ya kuchongewa krosi maridhawa na Shafiq Batambuze kutoka winga ya kushoto.

Dakika tisa baadae, Peter Manyika alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti lililokuwa likizama ndani baada ya Gor Mahia kufanya shambulizi langoni wa Singida United.

Licha ya Singida United kumuingiza Salum Chuku, Felipe Santos na Lubinda Mundia lakini bado walishindwa kuhimili vishindo vya Gor Mahia ambapo dakika ya 90 ya mchezo, mshambuliaji Meddie Kagere alitupia msumari wa mwisho baada ya kuachia shuti la chini chini lililomshinda golikipa Peter Manyika na kuiandikia Gor Mahia bao la pili.

Hadi mpira unamalizika kwenye dimba la Afraha, ni Gor Mahia waliotoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 ambapo sasa wanatarajiwa kupambana na Simba SC kwenye mchezo wa fainali utakaopigwa siku ya Jumapili Julai 10 huku singida wakitarajiwa kuchuana na Kakamega Homeboyz kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itakayopigwa mapema saa saba kamili mchana siku hiyo hiyo.


Spread the love

More in Habari