Connect with us

Habari

Gor Mahia Yailaza Simba 2-0 Na Kutwaa Ubingwa Wa SportPesa Super Cup 2018

Spread the love

NAKURU, Kenya –Mabingwa wa Kenya klabu ya Gor Mahia FC wamefanikiwa kutetea ubingwa wao wa michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kuilaza Simba SC kutoka nchini Tanzania kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali.

Mabao ya Meddie Kagere na Jacques Tuyisenge kipindi cha kwanza na cha pili yalitosha kabisa kulizamisha jahazi la Simba kwenye dimba la Afraha ambalo lilifurika rangi za kijani na nyeupe na kuwafanya magwiji hao wa soka Afrika Mashariki na kati kukata tiketi ya kwenda nchini Uingereza kucheza dhidi ya klabu ya Everton.

Kipindi cha kwanza

Mechi ilingóa nanga kwa visanga vya aina yake ambapo haikuwachukua Gor Mahia muda mrefu kuandika bao la kwanza lililofungwa na mshambuliaji hatari, Meddie Kagere mnamo dakika ya tano baada ya kumiliki mpira eneo la hatari, kugeuka na kuachia mkwaju wa chini chini uliomshinda golikipa Aishi Manula.

Kuingia kwa goli hilo kuliongeza hamasa kwa upande wa mabingwa hao watetezi ambao waliendelea kulishambulia goli la Simba kama nyuki.

Mshambuliaji wa Gor Mahia, Meddie Kagere (22) akishangilia baada ya kufunga goli la kwanza dhidi ya Simba kwenye fainali ya SportPesa Super Cup. (Picha/SPN)

Simba walijibu mapigo kwa shambulizi la kushtukiza ambapo pasi ya Jonas Mkude kutoka katikati ya uwanja ilimkuta Rashid Juma aliyeingia kwenye 18 ya Gor Mahia na kuachia shuti la chini chini ambalo lilipata hifadhi salama kwenye mikono ya golikipa Shaaban Odhoji.

Dakika 20 za mwanzo zilisheheni nguvu, kasi na ufundi wa hali ya juu huku wachezaji kutuniashana vifua hali iliyofanya nahodha wa Simba, Erasto Nyoni kuoneshwa kadi ya manjano huku dakika mbili baadae, nahodha wa Gor Mahia pia, Harun Shakava akilimwa kadi ya manjano na mwamuzi Tadesse Belay kutoka Ethiopia.

Almanusura Gor Mahia wapate bao la pili dakika ya 37 lakini Aishi Manula alisimama kidete kuokoa  mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na George Odhiambo maarufu kama Blackberry huku dakika chache baadae shuti la Francis Kahata likitoka nje ya lango la Simba sentimita chache baada ya wachezaji wa Gor Mahia kugongeana pasi murua.

Kipindi cha pili

Kipindi cha pili hakikuwa na mabadiliko makubwa ambapo Gor Mahia waliendelea kuwa tishio langoni mwa Simba na haikuwachukua muda mrefu kuandika bao la pili katika dakika ya 56 kupitia kwa Jacques Tuyisenge.

Jacques Tuyisenge (kulia) akishangilia pamoja na mchezaji mwenzake, Meddie Kagere (kushoto) baada ya kupachika kimiani bao la pili kwenye fainali ya SportPesa Super Cup (Picha/SPN)

Simba walifanya mabadiliko mfululizo ambapo waliwatoa Rashid Juma, Rashid Mohamed, Yusuf Mlipili na Shomari Kapombealiyeshindwa kuendelea na mchezo huku nafasi zao zikichukuliwa na Marcel Kaheza, Moses Kitandu, Shomary Ally pamoja nae Mohamed Ibrahim.

Gor Mahia nao walifanya mabadiliko kadhaa ambapo waliwatoa Meddie Kagere, Humphrey Mieno na George Odhiambo huku nafasi zao zikichukuliwa na Lawrence Juma, Innocent Wafula na Boniphace Omondi

Na hadi dakika 90 zinamalizika, Gor Mahia waliibuka wababe kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 na kutetea ubingwa wao huku pia wakikata tiketi ya kucheza na Everton kwenye mchezo wa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi utakaopigwa kwenye dimba la Goodison Park nchini Uingereza.

Tuzo Binafsi

Mbali na ubingwa huo lakini wachezaji wa Gor Mahia waliweza kung’aa kwenye tuzo binafsi ambazo zilitolewa na waandaaji wa michuano hiyo, kampuni ya SportPesa.

Mlinzi Philemon Otieno aliibuka mchezaji bora wa mechi ya fainali ambapo alikabidhiwa kitita cha Dola 500 sawa na zaidi ya Shilingi Milioni 1.2 za kitanzania.

Mshambuliaji wa Gor Mahia, Meddie Kagere (kulia) akipokea tuzo ya mfungaji bora wa michuano ya SportPesa Super Cup kutoka kwa muwakilishi wa klabu ya Everton (Picha/SPN)

Meddie Kagere aliweza kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa mashindano baada ya kupachika mabao manne kimiani sambamba na tuzo ya mchezaji bora wa jumla wa mashindano (MVP) huku Shaaban Odhoji Wa Gor Mahia pia akitwaa tuzo ya golikipa bora wa mashindano baada ya kutoruhusu nyavu zake kutikiswa kwenye michezo yote.

Hongereni Gor Mahia, tukutane tena mwakani!


Spread the love

More in Habari