Connect with us

Habari

Giroud Aibuka Shujaa Huku Arsenal Ikifungua Pazia La EPL Kwa Kuitandika Leicester City Mabao 4-3

Spread the love

LONDON, Uingereza -Mabingwa wa kombe la FA na ngao ya hisani klabu ya Arsenal imeibuka na ushindi wa mabao 4-3 kwenye mechi ya ufunguzi wa ligi Kuu nchini Uingereza dhidi ya Leicester City.

Arsenal ikiwa kwenye dimba lake la nyumbani la Emirates, ilibidi isubiri hadi dakika za majeruhi kuweza kuibuka na ushindi huo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-2 hadi kufikia dakika ya 83 ya mchezo dhidi ya vijana wa kocha Craig Shakespeare.

Iliwachukua Arsenal dakika mbili tu kuandika bao la uongozi mara tu baada ya mchezo kuanza lililofungwa na mshambuliaji mpya, Alexandre Lacazette aliyeunganisha kwa kichwa krosi maridadi iliyochongwa na Mohamed Elneny na kuipa Arsenal bao la kuongoza ambalo hata hivyo halikudumu sana kwani dakika tatu mbele, Shinji Okazaki alitumia vyema makosa ya walinzi wa Arsenal walioshindwa kuondosha katika hatari mpira uliorudishwa kwa kichwa na Henry Maguire na kumfanya Okazaki kuandika bao la kichwa kwa upande wa Leicester.

Jamie Vardy aliiandikia Leicester City bao la pili dakika ya 29 ya mchezo akimalizia krosi maridhawa iliyopigwa na kiungo Marc Albrighton kutoka magharibi mwa uwanja na kufanya matokeo kuwa 2-1 lakini zikiwa zimesalia sekunde chache mpira kwenda mapumziko, Danny Welbeck akaiandikia Arsenal bao la kusawazisha baada ya kumegewa pande murua na mlinzi mpya wa kushoto, Sead Kolasinac na hadi mpira unakwenda mapumziko timu zote mbili zilikuwa zimefungana mabao 2-2.

Jamie Vardy akiiandikia Leicester City bao pili likiwa ni bao la kwanza kati ya mawili aliyofunga dhidi ya Arsenal kwenye dimba la Emirates

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Arsenal wakitawala sehemu kubwa ya mchezo ingawa alikuwa ni Jamie Vardy tena aliyezichungulia nyavu za Petr Cech kwa mara nyingine baada ya kuandika bao mnamo dakika ya 56 akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliochongwa nae Riyad Mahrez.

Arsene Wenger alifanya mabadiliko ambapo alimtoa Mohamed Elneny na nafasi yake kuchukuliwa na Aaron Ramsey kisha akatoka mlinzi Rob Holding na nafasi yake kuchukuliwa na Olivier Giroud dakika ya 67 lakini hata hivyo iliwabidi wasubiri hadi dakika ya 83 ili kuweza kusawazisha bao baada ya Aaron Ramsey kuunganisha pasi ya Granit Xhaka kwa shuti la chini chini lililomshinda kipa Kasper Schmeichel wa Leicester City.

Dakika mbili baadae, Olivier Giroud aliunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Granit Xhaka na kuifungia Arsenal bao la ushindi huku ubao wa matokeo ukisomeka 4-3

Olivier Giroud akishangilia baada ya kuiandikia Arsenal bao la ushindi dakika ya 85 kwa kichwa dhidi ya Leicester City

Hadi mwamuzi Mike Dean anapuliza kipenga cha mwisho kuashiria kumalizika kwa mchezo, Arsenal walikuwa mbele kwa mabao manne huku Leicester wakibakia na mabao yao matatu.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo kadhaa itakayopigwa kwenye viwanja mbalimbali nchini humo ambapo mechi ya mapema itakuwa ni kati ya Watford na Liverpool itakayopigwa majira ya saa nane na nusu mchana na kisha baadae mabingwa watetezi Chelsea watawakaribisha Burnley kwenye dimba la Stamford Bridge, Crystal Palace watakuwa wenyeji wa Huddersfield Town, Everton wakiwakaribisha Stoke, Southampton wakiwa wenyeji wa Swansea, West Bromwich Albiol wakicheza na Bournemouth na huku mechi ya mwisho ikiwa kati ya Brighton & Hove Albiol watakaokuwa wenyeji wa Manchester City.


Spread the love

More in Habari