Connect with us

Habari

Baada Ya Dhoruba Ya Jana; Je, Yajayo Yatafurahisha? Simba Watatupa Majibu Kamili Leo

Spread the love

NAKURU, Kenya -Ilikuwa ni jioni ndefu kwa mashabiki ambao huwa hawawezi kula wala kunywa wakisikia neno soka limekatiza masikioni mwao na hata jua lilipozama bado kivuli cha Uwanja wa Afraha kiliendelea kuitesa Tanzania.

Bila shaka mang’amung’amu ya Kakamega Homeboyz na Gor Mahia yaliendelea kuwawinda wengi usingizini huku wakishindwa kuelewa kinagaubaga.

Haikuwa siku nzuri kwa watanzania waliopo mjini Nakuru kushuhudia michuano ya SportPesa Super Cup kwani uwakilishi wa Yanga na JKU uliota mbawa na kuwaacha Wakenya wakirindima kwa shangwe, hoi hoi, nderemo na vifijo.

Mapema tu, Yanga walibwaga manyanga mbele ya Kakamega kwa kumruhusu mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Allan Wanga kuwaadhibu huku JKU nao wakishindwa kuhimili dhoruba za Gor Mahia.

Kama ungefaniwa kuliona basi lililobeba mashabiki wa Gor Mahia wakati wakitoka uwanjani jinsi lilivyokuwa likinesanesa kwa madaha kwenye barabara za mjini hapa basi ni lazima roho ingekuuma wewe ukiwa kama mtanzania, achilia mbali shabiki wa JKU au Yanga.

Yanga

Yanga walijitahidi kucheza lakini umakini wa safu ya ulinzi na utumiaji wa nafasi ulikuwa ukiwavuta shati bila kusahau jinsi mzimu wa msimu mbaya wa VPL ulivyokuwa ukiwawinda mchana kweupe.

Wachezaji hawakuwa wakionekana kutafuta magoli kwa nguvu tofauti na wapinzani wao huku mabeki wa pembeni Hassan Kessy na Haji Mwinyi wakishindwa kabisa kujaza majalo ndani hali iliyofanya washindwe kushambulia kupitia pembeni.

Kuingia kwa Ajib kulirudisha matumaini kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira lakini kwa upande mmoja hali hiyo iliwaumiza Yanga kutokana na jinsi ambavyo alikuwa akipoteza pasi kila wakati.

Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib akiwatoka walinzi wa Kakamega Homeboyz kwenye mchezo wa robo fainali ya SportPesa Super Cup hapo jana ambapo Yanga ililala kwa mabao 3-1 (Picha-SPN)

Wapo waliosema Ajib hakuwa fiti kucheza lakini binafsi sidhani kama hilo ni tatizo kwani hiyo sio sababu ya kumfanya apoteze mipira kila mara pale ilipoonekana anaweza kutoa pasi kwa mwenzake

Yaliyopita si ndwele lakini bila shaka uwepo wa Kamusoko, Tshishimbi na Makapu ungeleta uzoefu mkubwa kwenye kiungo cha Yanga kama watu hawa wangeanza pamoja huku Ajibu, Tambwe na Mahadhi wakipeleka mashambulizi mbele. Ni maoni yang utu!

JKU

Ingawa kwa muda fulani mchezo ulionekana kuwa sawia, lakini hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu mpaka pale Francis Kahata alipochomoa makucha yake kwenye eneo la kiungo cha kati cha Gor Mahia.

Mshambuliaji wa Gor Mahia, Meddie Kagere akishangilia goli aliloifungia time yake dhidi ya JKU kwenye ushindi wa mabao 3-0 hapo jana (Picha-SPN)

Yule bwana mdogo aliwapoteza kabisa JKU katikati na ilifika muda alikuwa akionekana yeye tu huku akipiga pasi maridhawa zenye macho, akimiliki mpira kwa kujiamini na kusogea mbele kwa nafasi.

JKU walizidiwa kila kitu hali iliyomfanya kocha Hassan Ramadhani kukiri kuwa hawakuwa na la kufanya kwani kupindua matokeo dhidi ya kikosi cha Gor Mahia ambacho kilikuwa kimezungukwa na wazoefu kila idara lilikuwa ni jambo gumu.

Yajayo yanafurahisha?

Baada ya kuwaona mashabiki wa Yanga waliofika uwanjani wakiwa wamechelewa kwenye mechi ya jana huku wakikaribishwa kwa kipigo na kutakiwa kurudi nyumbani kabla hata hawajayaonja mema ya mji huu, swali ni je, yajayo yanafurahisha?

Simba leo anashuka dimbani majira ya sita kamili mchana kupambana na Kariobangi Sharks ambao kwa upekenyuzi wangu wa hapa na pale nimeambiwa ni timu iliyosheheni vijana waliolelewa kwa pamoja tangu wakiwa wadogo.

Sifahamu kuhusu Sharks zaidi ya kujua tu kwamba walimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimu wa Ligi Kuu Kenya uliomalizika wa 2016/17 nyuma ya Gor Mahia na Sofapaka lakini ninachojua ni kuwa Simba ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania bara wakiwa na wachezaji mahiri.

Kubadili mfumo

Sina uhakika na jinsi walivyowaacha wachezaji wao bora nyumbani hali inayomfanya Mfaransa Pierre Lechantre kukiri kuwa analazimika kubadili mfumo wa uchezaji alipokuwa akiongea na wana habari hapo jana.

Kocha wa Simba, Pierre Lechantre akizungumza na wana habari Juni 3 kuelekea mchezo wao wa robo fainali dhidi ya Sharks (Picha-SPN)

“Nitabadili aina ya mchezo wetu ili iendane na wachezaji tuliokuja nao hapa. Ni pigo kwetu kuwakosa wachezaji kama Emmanuel Okwi na John Bocco. Ni wachezaji muhimu lakini wameshindwa kuja kutokana na sababu mbalimbali. Tutatazama wachezaji waliopo hapa wanaweza kufanya nini”, alisema Lechantre.

Sina uhakika sana katika hili lakini ninachojua ni kuwa karibia msimu mzima Simba wamecheza 3-5-2 na ndio mfumo ulitufanya tuwaone wakiwa imara zaidi.

Bila ya uwepo wa Okwi, Bocco, Gyan, Kwasi na Kotei ambao walikuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza, nasubiri kuona jinsi Simba watakavyocheza leo ingawa bado naamini watu kama Niyonzima, Ndemla, Kapombe na nahodha Zimbwe Jr wataweza kufanya makubwa.

Simba wamebeba matumaini ya watanzania mabegani mwao leo lasivyo utawala wa timu za Kenya kwenye michuano hii utazidi kuota mizizi.

Tusubiri tuone kama yajayo yanafurahisha baada ya wingu zito la jana kuendelea kuitawala tasnia ya soka kwa ngazi ya vilabu nchini.

Tukutane Afraha!


Spread the love

More in Habari